
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Yn.6:52
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu baada ya kueleza juu ya yeye kuwa chakula cha uzima na kwamba chakula anachotoa kwa ajili ya ulimwengu ni mwili wake, Wayahudi walishangazwa na kauli hii na kuanza kuhojiana wao kwa wao kuhusu uwezekano wa neno hili.
- Jambo hili hata lingekuwa katika nyakati zetu bado tungeendelea kuulizana au kushindania kile alichosema Yesu kwa sababu si jambo la kawaida kwa mtu kutoa mwili wake kwa ajili ya kuwa chakula cha wengine. Pamoja na hali hiyo Wayahudi hawakudhubutu kumuuliza Yesu aliyesema maneno haya.
- Je, ni mara ngapi unalisikia neno kutoka kwenye maandiko na ndani yako unakosa uhakika au tafsiri sahihi kiasi kwamba unakata tamaa ya kumtafuta Mungu. Yako maneno mengi ndani ya biblia ambayo yametatiza sana watu wengi kiasi cha kushindwa kumfuata Yesu.
- Wewe unapotatizika na maandiko au neno lililonenwa kwenye maandiko unaenda wapi au unahojiana na nani? Kwa hakika chanzo kikubwa cha uwepo wa madhehebu mengi katika dini ya ukristo ni utofauti wa tafsiri za kimaandiko baina ya watu mbalimbali.
- Hali ya uwepo wa madhehebu mengi inatokana na sisi wanadamu kubeba tafsiri zetu wenyewe kuhusiana na neno la Mungu badala ya kumuuliza Mungu kuhusiana na kile kinachosemwa na neno lake.
- Kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho na kuonya watu na kuwadibisha katika haki ili kuwakamilisha watu wa Mungu. Maandiko yanaeleza juu ya neno la Mungu kusimama imara siku zote katika mazingira yote.
- Hatuna haja ya kushindana au kubishana kile ambacho kimesemwa katika neno la Mungu ila tunayo nafasi ya kumuuliza aliyesema yaani Yesu Kristo mwenyewe. Ndio maana aliahidi kumleta Roho Mtakatifu ili atuongoze kwenye kuijua kweli yote.
- Usikubali kuyumbishwa na tafsiri za watu au hoja za kibinadamu kuhusiana na neno la Mungu, mtafute Mungu mwenyewe atakuongoza katika kuijua kweli yote katika maisha yako ya kumfuata.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!