Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu’ Yn.6:51
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu anaendelea kusisitiza juu ya Yeye kuwa chakula cha uzima kwa ajili ya watu wote au ulimwengu mzima. Hii ni habari njema kwa ajili ya kila mwanadamu. Yesu ni chakula kwa ajili yetu, chakula pekee kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya kila mmoja wetu.
- Bwana Yesu anaeleza wazi kabisa ya kuwa chakula anachotoa kwa ajili ya ulimwengu ni mwili wake. Jambo hili ni la kushangaza kabisa kwani si kawaida kwa mwanadamu kutoa mwili au mwanadamu mwengine kula mwanadamu. Kwa kawaida hakuna uhalali wa mtu kumla mtu mwengine. Lakini hapa Bwana Yesu anatupa ufahamu wa ndani kuhusiana na masuala ya kiroho ya kuwa tunahitaji kumla Yeye kwa ajili ya kupata uzima.
- Chakula hiki anachosema kuwa mwili wake ana maana ya kula Neno lake. Kwa maandiko tunafahamu ya kuwa utambulisho wa Bwana Yesu kabla hajaja duniani alikuwa anatambulika kama Neno hii ni kwa mujibu wa Yn.1.1-4. Na kwamba sisi wote na viumbe vyote tumefanyika kupitia Yeye. Hivyo njia pekee ya kufikia makusudi yale ambayo tumetumwa hapa duniani ni kuishi ndani yake Neno.
- Kitendo cha mtu kujiita mwamini katika Kristo lakini hana muda wa kusoma na kujifunza neno la Mungu huku akilitekeleza ni kujidanganya mwenyewe. Asili yetu, maisha yetu na hatma yetu inategemea kwa kiasi kikubwa kuambatana kwetu na Neno.
- Mwili wa Yesu Kristo tayari ulishatolewa kwa ajili yetu pale msalabani, na kwamba kila siku ipo sehemu yetu ya kupata chakula hiki ili tuendelee kuishi hata milele katika kumjua Mungu.
- Kama tulivyojifunza ya kuwa uzima wa milele si suala la kuishi tu maisha daima pasipo kifo bali ni uwezo wa kimungu ndani yetu katika kumjua Mungu na Yesu Kristo. Kwa kadri tunavyoendelea kupata neno lake kila siku ndivyo tunazidi kumjua na kufananishwa naye katika mambo yote.

- Hakuna siku tutakayoweza kusema tumetosheka na neno la Mungu kwani maisha yetu yanatarajia kile kinachotoka katika kinywa cha Mungu kwa ajili yetu kila siku na si mkate au chakula cha mwili peke yake.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!