
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu’ Yn.6:51
Mambo ya kujifunza
- Katika andiko hili tunaona kwa mara nyingine Bwana Yesu anajitambulisha kama chakula cha uzima kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya ulimwengu mzima. Hili ni neno zito sana ambalo tunapaswa kulielewa.
- Yesu Kristo hakuja duniani kwa ajili ya wayahudi au wakristo peke yao bali kwa maneno haya anadhihirisha ya kuwa alikuja kwa ajili ya ulimwengu mzima. Ndio maana maandiko yanaeleza juu ya Mungu kuupenda ulimwengu kiasi cha kumtoa mwana wake wa pekee. Yn.3.16.
- Historia inatuonesha juu ya mazingira aliyowatunza Mungu wana wa Israel jangwani kwa kipindi cha miaka 40 kwa kuwalisha mana iliyotoka mbinguni. Tunaambiwa ya kuwa yale yaliyofanyika katika Agano la Kale yalikuwa ni kivuli kwa ajili ya picha halisi ya Agano Jipya ndani ya Yesu. Ile mana inafananishwa na neno la Kristo ambalo tunapaswa kulipokea kila siku.
- Baba zetu waliila mana kule jangwani kwa miaka 40 lakini hatimaye walikufa kimwili na wengi wao hawakuweza kuingia Kanaani bali watoto wao walioamini njia ile Mungu aliyokuwa akiwapitisha. Sisi nasi tupo safarini hapa duniani hatuna mji udumuo na tunapokea neno la Kristo kama mana waliyopokea baba zetu.
- Uamuzi wa kufika Kanaani au kutokufika ni wetu binafsi wala si wa Mungu. Tukumbuke kama baba zetu walivyotolewa Misri kwa ishara na maajabu makubwa, wote walitoka lakini si wote waliomaliza safari. Sisi nasi tumeokolewa kwa neema kwa kumwamini Yesu Kristo kwa kusikia sauti yake ya kututoa kwenye utumwa wa dhambi, lakini ili kuingia Kanaani yetu tunamuhitaji Yesu na neno lake kila siku na kila saa tusifie jangwani.
- Tunaposoma na kuona uasi na ukaidi wa wana wa Israel wakati wakiongozwa na Musa tunawashangaa. Lakini pia sisi ndivyo tulivyo, hatumkubali Yesu kwa ukamilifu wa mioyo bali tunataka mambo yetu wenyewe na njia zetu wenyewe. Wengi wamechoka na safari hii na wamekata tamaa na kufanya shauri la kurudi Misri, yaani kuishi maisha yale ya awali ya uasi na dhambi. Je, mimi na wewe ni miongoni mwao?
- Tunayo kila sababu ya kumwamini Yesu Kristo na kumtegemea kama chakula cha uzima cha kweli kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu. Ndio chakula kinachoweza kutusaidia na kutuvusha katika magumu yote tunayopitia jangwani na kutufikisha salama katika Kanaani yetu. Kamwe tusifikiri kumwasi BWANA kwa maana hakika tutaangamia wote.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!