Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tulianza kuangalia habari ya nafasi ya muujiza katika maisha ya kiimani. Tumejua ipo tofauti ya vyanzo vya miujiza na suala la msingi ni kutazama muujiza kama ishara na ujue inakupeleka wapi.
Leo tunaendelea kujifunza zaidi juu ya sababu ya muujiza wa kulisha watu 5,000 kwa mikate 3 na samaki 2. Karibu sana tuendelee kujifunza.
‘Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula mikate mkashiba’ Yn.6:26
Ufafanuzi
- Hili ni swali la msingi sana la kujiuliza kwa watu na waamini kila siku. Kwa sababu gani unamtafuta Yesu. Wengi wanamtafuta Yesu ili awatimizie mahitaji yao ya kimwili. Una shida ya chakula, au shida ya mavazi, au shida ya kifedha au shida ya ugonjwa n.k.
- Mkutano waliopata kula chakula cha Yesu, waliona kuwa sasa hali ya maisha yao imebadilika. Wakaamua kuingia gharama hata ya kusafiri kwenda mahali Yesu alipo wakijua haja ya miili yao yaani chakula ataitimiza. Wewe umeingia gharama kiasi gani mpaka sasa kumtafuta Yesu? Je, kuna kitu gani Yesu amefanya kwenye maisha yako ya kimwili kiasi kwamba kimekushikilia unamfuata kila wakati? Yesu asipokupatia kitu cha kimwili unachokitafuta kwake, utaacha kumfuata au?
- Angalia sana watu wanaokuhubiria kila uchao wanakuahidi mambo gani kutoka kwa Yesu. Wahubiri wengi wameibadili injili ya Kristo na kuifananisha na vitu vya dunia yaani materialistic gospel. Wanatoa ahadi za watu kubarikiwa, kuinuliwa, kupata fedha, safari za ulaya, wachumba, magari, nyumba, biashara, huduma etc hayo ndiyo makutano wanapenda kusikia na wahubiri wanapenda kuwaambia kile watu wanataka kusikia.
- Wengi wanakoseshwa kwa kuhubiriwa Yesu wa vitu vya kimwili badala kusudi la Yesu la kiroho kwa kila mtu. Hii haimaanishi kuwa Yesu hayapi uzito mahitaji yetu ya kimwili bali anasema lengo/focus ni kuutafuta kwanza ufalme wake na haki yake hayo mengine – ya kimwili ni ziada. Wahubiri wanawakosesha watu katika kutafuta vile vya ziada badala vya msingi.
- Yesu anawaambia mkutano, ninyi mnanitafuta si kwa sababu mliona ishara bali ni kwa sababu mlikula mikate mkashiba. Hatuwezi kumdanganya Mungu au kumfuata kwa unafiki, kwani anaijua mioyo yetu siku zote ni kitu gani tunakifuata kwake. Wale makutano waliingia gharama na walipomwona wakamwita Rabi yaani Mwalimu ingawa kwao hakuwa mwalimu wala hawakujifunza kitu. Watu wanamwita Yesu Bwana, mkombozi, kiongozi,n.k lakini ndani ya mioyo yao Yesu hana nafasi hiyo ya kuwa Bwana au mkombozi au kiongozi bali ana nafasi nyingine kama Mlishaji au mfadhili basi.
- Hivyo kila wakati unapotaka kuchukua hatua yoyote ya kumfuata Yesu, jiulize ni kwa nini namtafuta. Iwe kwenye kusoma neno, au kusikiliza mahubiri, au kwenda ibadani, au kwenye maombi au kwenye matendo yoyote ambayo unafanya kwa nia ya kumtafuta Yesu, jiulize kwa nini unamtafuta.
Mungu wetu atusaidie katika kutafakari maneno haya na kutusaidia kusikia sauti zinazoambatana na miujiza au ishara ikiwa zinatuelekeza kwake au la na kujifunza kuchukua hatua sahihi ndani ya Kristo.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
Wako katika Bwana Yesu Kristo
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Je, kwa nini unamtafuta Yesu?
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!