
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Baba zenu waliila mana jangwani wakafa’ Yn.6:49
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu anawakumbusha wayahudi juu ya historia ya baba zao walipotoka Misri na kuingia jangwani kwa safari ya Kanaani. Mojawapo ya muujiza mkubwa Mungu alioufanya katika safari hii ya miaka 40 ni kuhakikisha wana wa Israel wanapata chakula kila siku.
- Mungu alimpa maagizo Musa kwa ajili ya wana wa Israel ya kuwa kila siku asubuhi kabla ya kuchwa watoke nje na kuokota chakula ambacho Mungu anawapatia na yakuwa siku ya 6 wataokota mara 2 zaidi ili siku ya 7 wasitoke kuokota. Maagizo haya waliyashika kwa takribani miaka 40. Lakini tunafahamu hatma ya wana wa Israel hawa hawakuingia Kanaani pamoja na kupata chakula kile wakati wa safari yao. Wengi walikufa jangwani. Ni watu 2 pekee ndio walioanza safari kutoka Misri na kufika Kanaani miongoni mwao yaani Yoshua na Kalebu. Soma zaidi Hes.14.
- Hapa tunajifunza ya kuwa kipo chakula ambacho unaweza kupata lakini kisikupe uhakika wa maisha na kumaliza safari uliyokusudiwa. Haikuwa mpango wa Mungu kuwatoa Misri na wafie jangwani ila kwa sababu ya uasi wao na kutokumwamini Mungu ndivyo walishindwa kuingia Kanaani.
- Hapa tunajifunza ya kuwa Mungu anaweza kukutoa katika utumwa kule Misri lakini sio ‘guarantee’ ya wewe au mimi kufika Kanaani kule Mungu alikokusudia. Si kwamba Mungu anashindwa kutufikisha bali itategemea imani yetu juu ya huyu Mungu. Wapo watakaofika lakini pia wapo watakaoshindwa kufika.
- Tunaweza kupata ‘mana’ kwa ajili ya kutusaidia katika safari, je tutaendelea kumtegemea Mungu kila siku, tutakuwa na utii wa neno lake na maagizo yake kila siku? Hapa ndipo mtihani mkubwa upo kwa ajili yetu. Fikiria safari ya wana wa Israel ni watu wawili tu walioweza kutoka mwanzo wa safari hadi mwisho kati ya wale waliokuwa na umri kuanzia miaka 20, wengi walioingia Kanaani ni wale waliozaliwa jangwani.
- Yesu Kristo anatuonya ya kuwa baba zetu walikula mana lakini walikufa, je sisi tunataka kuwa hai na kufika mwisho wa safari yetu salama? Tuna kila sababu ya kumsikiliza kila hatua ya maisha yetu hata kama tutapitia mambo magumu.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!