Day.33. Spiritual Food: Je, ni nani chanzo chako cha taarifa kuhusu Mungu?
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba’ Yn.6:46
Mambo ya kujifunza
- Maneno haya anayasema Bwana Yesu ya kwamba hakuna mtu aliyemwona Baba yanatupa tafakari sana kuhusu taarifa tunazopokea kutoka kwa vyanzo mbalimbali. Kabla ya Yesu kuja katika mwili tulikuwa tunapata taarifa kuhusu Mungu kutoka kwa watumishi mbalimbali. Lakini baada ya Yesu kuja katika mwili anatueleza habari halisi za Mungu.
- Duniani kwa sasa kuna watu wengi sana wanazungumzia juu ya miungu mbalimbali na jinsi inavyoweza kufanikisha watu mbalimbali. Watu wanatoa shuhuda nyingi kuhusu miungu wanayoisikia kila siku.
- Yesu Kristo anatueleza wazi wanadamu wote ya kuwa hakuna mtu amemwona Baba yaani hakuna mwanadamu aliye hai anamjua Mungu kwa ukamilifu wake isipokuwa Yeye pekee Yesu Kristo aliyemwona Mungu na mwenye asili ya Mungu. Hii ina maana tukitaka kupata uhakika juu ya uhalisia wa Mungu tunapaswa kumsikia na kumfuata Yesu katika mambo yote.
- Ni kweli sisi wanadamu tunaweza kupata kufahamu kwa sehemu kiasi kile tulichofunuliwa na Mungu kuhusiana na uhalisia wake na ndivyo tunavyoshikirishana kila inapopatikana nafasi. Lakini hakuna mwanadamu anayemjua Mungu kwa uhalisia wote kwa ujumla. Ni Yesu peke yake aliye Mungu wa kweli aliyeshuka kwa ajili yetu.
- Je, mimi na wewe tunasikiliza taarifa zipi au chanzo kipi cha taarifa kuhusiana na Mungu? Ili tuweze kujenga uhusiano imara kila siku ndani ya Mungu ni lazima tumsikie Bwana Yesu kile anachosema nasi kwa neno lake.
- Ndio maana Bwana Yesu alitoa agizo kwa wanafunzi wake kuenenda duniani kote kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wa Yesu na kuwafundisha yale yote aliyoyaamuru. Hii ina maana kama tunataka kufika kwa Baba hatuna budi kujifunza kila kitu kutoka kwa Yesu Kristo na kufuata kile alichoamuru. Baada ya Yesu Kristo hakuna mtume au nabii ambaye ni mkuu kuliko Kristo anayeweza kuleta njia mpya ya kufika kwa Mungu. Ndio maana alisema kila kitu kinaweza kupita ila maneno yake yadumu milele.

- Hakikisha Bwana Yesu anakuwa chanzo cha taarifa kumuhusu Mungu wako ili kuwa na uhakika wa safari yako.
MAOMBI LEO
Ikiwa ndani yako ungependa kuona ahadi ya Bwana Yesu inatimia ya kuwa usipotee milele bali upate kufufuliwa siku ya mwisho na kwamba unaona uhusiano wako kwa sasa na Bwana Yesu si sahihi na unashuhudiwa moyoni ya kuwa endapo leo ni siku yako ya mwisho kuna uwezekano wa hukumu, basi chukua hatua na kubadili mkondo wa historia yako kwa kusali pamoja name
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!