Day.31. Spiritual Food: Yesu ndiye Ufufuo

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho’Yn.6:44
Mambo ya kujifunza
- Kati ya mambo mazito yanayomtatiza mwanadamu yeyote ni suala la kifo. Kifo kimekuwepo tangu mwanadamu wa kwaza kufa kimwili yaani Habili aliyeuwawa na ndugu yake Kaini. Kifo ni matokeo ya dhambi yetu ya asili ndani ya Adamu.
- Kifo hakizoeleki hata siku moja kwani kila siku kinapotokea ni kipya kwetu na si rahisi kwa manadamu kukabiliana nacho. Ni watu wengi kwenye historia waliokuwa maarufu na kufanya mambo makubwa lakini hakuna aliyeweza kustahimili juu ya kifo.
- Kuna ukweli katika maisha ya kila mmoja wetu ya kuwa kama ilivyo siku ya kuzaliwa basi ni lazima ipo siku moja tutakufa katika mwili huu. Huu ndio ukweli wa maisha. Ni kweli pia kila sekunde mimi na wewe tunayoitumia, yupo mtu ambaye ndio sekunde yake ya mwisho. Swali muhumu kwetu, je tunaitumia vipi pumzi hii ambayo ipo siku, saa, dakika na sekunde tusiyoijua PUMZI HII ITAONDOLEWA kwetu?
- Lakini sisi tunaomwamini Yesu tunalo tumaini jema na Baraka katika Kristo ambaye katika historia ya mwanadamu tangu kuumbwa kwa ulimwengu ni yeye pekee aliyezaliwa katika mwili, akafa, akazikwa na siku ya tatu akafufuka na mpaka sasa YU HAI. Hakuna mwanadamu mwenye historia hii popote katika vitabu vya maandiko ya dini yoyote au imani yoyote.
- Mimi na wewe tunaitwa na Baba kumwendea Yesu kwa imani ya kufufuliwa na kuishi katika uzima ndani yake. Itoshe kusema kuwa hakika ya maisha yetu baada ya kifo ipo ndani ya Yesu Kristo. Tukimkubali na kuikubali dhabihu yake msalabani sasa tunapata maisha ya uzima wa milele ndani yake.
- Ni maombi yangu Mungu akujalie neema ya kumkubali Yesu LEO maana ndio siku ya wokovu wako.
MAOMBI LEO
Ikiwa ndani yako ungependa kuona ahadi ya Bwana Yesu inatimia ya kuwa usipotee milele bali upate kufufuliwa siku ya mwisho na kwamba unaona uhusiano wako kwa sasa na Bwana Yesu si sahihi na unashuhudiwa moyoni ya kuwa endapo leo ni siku yako ya mwisho kuna uwezekano wa hukumu, basi chukua hatua na kubadili mkondo wa historia yako kwa kusali pamoja name
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!