Day.30. Spiritual Food: Acha Kunung’unika

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Basi Yesu akajibu akawaambia, msinung’unike ninyi kwa ninyi’Yn.6:43
Mambo ya kujifunza
- Ni tabia ya watu wengi kupenda kunun’gunika au kulalamika mara kwa mara. Hii ni kwa sababu tunaona tumeonewa au haturidhiki na hali yetu.
- Yesu alikuwa akiwaeleza ya kuwa yeye ni chakula cha uzima hili ni neno la kiroho, lakini kwa kutokuelewa kwao wakaanza kunun’gunika kila mmoja aliyesikia neno hili. Kuna mambo mengi Bwana Yesu anasema katika maisha yetu binafsi au kama Kanisa au jamii lakini watu kwa kutokuelewa huanza kunung’unika na kulalamika.
- Tunasahau ya kuwa ni Yesu ndiye aliyetoa ujumbe lakini tunaanza kulalamikiana sisi kwa sisi. Utakuta waumini wanamlalamikia mtumishi kana kwamba neno lililosemwa ni lake binafsi. Wapo watu ambao Mungu akisema nao na wao wakiona kuwa hawawezi kuamini neno hilo basi hufikiri kila mtu hapaswi kuamini.
- Mfano maandiko yanaeleza juu ya walioamini kuwa na mfumo wa maisha matakatifu wakiwa hapa duniani ili kumwona Mungu. Lakini kwa kutokuelewa dhana au ukweli wa aina ya maisha hayo, watu wanasema kamwe haiwezekani mwanadamu kuishi maisha ya utakatifu hapa duniani. Na hali hii imeanza kukubaliwa hata ndani ya Kanisa ya kuwa haiwezekani na hivyo kuondoa msisitizo wa mafundisho hayo katika mwenendo wa maisha ya waamini.
- Ikiwa hatujaelewa kile Yesu anachosema nasi basi tuwe na moyo wa ujasiri wa kumwomba atufunulie kwa msaada wa Roho Mtakatifu maana ndiye mwenye kutongoza katika kweli yote ili tusije kupotosha maandiko na kukwaza watu wengine. Kushindwa kwako kuamini na kuishi kile Yesu anachosema kusizuie wengine wanaotaka kumfuata kwa ukamilifu.
- Ni lazima tufahamu ya kuwa Mungu habadiliki wala hana upendeleao, vigezo alivyoweka vya mahusiano yake na watu havibadiliki. Kulalamika au kunung’unika hakuwezi kutaua changamoto hizo bali hupofusha fikra za kuona namna bora ya kutii neno la Mungu.
- Tujifunze kumwendea Yesu katika kila neno tusiloweza kulitii ili atuongoze na kutuonesha neema yake ya kutusaidia kukubali anachosema kwa ajili ya maisha yetu.
MAOMBI LEO
Inawezekana ndani yako umekuwa ukipambana katika kuishi maisha ya kumpendeza Mungu lakini vipo vizuizi ambavyo kila siku vinakuzuia na kukurudisha nyuma, usikate tamaa kila mmoja wetu anapitia changamoto katika kumfuata Yesu hivyo fuatana nami katika sala hii ya kukutia nguvu zaidi
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu wa kushindwa kukutii neno lako. Mara kwa mara ninaanguka lakini wewe wa rehema unaniinua. Ninaomba toba pale ambapo nimekata tama na kuendelea kuishi maisha yasiyokupendeza. Ninaomba neema yako na msaada wa Roho wako Mtakatifu uliyemleta ndani yangu anitie nguvu katika kulisikia neno lako na kulitii siku zote za maisha yangu. Asante kwa msaada wako na upendo wako wa kuniwezesha kuishi maisha ya kukupendeza wewe. Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!