Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tulianza kuangalia habari ya nafasi ya muujiza katika maisha ya kiimani. Tumejua ipo tofauti ya vyanzo vya miujiza na suala la msingi ni kutazama muujiza kama ishara na ujue inakupeleka wapi.
Leo tunaendelea kujifunza zaidi juu ya sababu ya muujiza wa kulisha watu 5,000 kwa mikate 3 na samaki 2. Karibu sana tuendelee kujifunza.
‘Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula mikate mkashiba’ Yn.6:26
Ufafanuzi
Muujiza wa kulisha watu mikate kama ishara
Kwa kutazama habari ya kulisha wanaume 5,000 tunaweza kujifunza mambo kadhaa ambayo Yesu alitaka makutano na wanafunzi wake tuweze kuona ishara hiyo ilikuwa na malengo gani.
Tunaona Yesu akienda Tiberia na mkutano mkuu ukamfuata kwa sababu waliona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye akakusudia kufanya ishara nyingine ya kuwapatia chakula mkutano mkuu kupitia mikate 5 na samaki 2. Wanafunzi wake waliona kuwa hata wakinunua chakula hakitatosha na samaki 2 kwa mikate 5 si kitu chochote mbele ya mkutano mkuu.
Kupitia mikate 5 na samaki 2 Yesu alilisha mkutano mkuu yapata wanaume 5,000 pasipo kuhesabu wanawake na watoto.
Mambo ya kujifunza
Je, ni mambo gani ambayo Mungu alikusudia wajifunze kutokana na muujiza wa mikate 3 na samaki 2? Je, ni maelekezo gani au ujumbe gani uliashiriwa na Bwana Yesu katika muujiza huu?

Tunaweza kuona mambo kadhaa ambayo tunajifunza ndani ya muujiza wa kulishwa watu 5,000
- Mungu anajua na kutambua uhitaji wetu wa kiroho na kimwili wakati wote tunapomfuata na yeye yu tayari kukidhi haja zetu.
- Katika kile kidogo kilichopo Yesu anaweza kukifanya kuwa tele kwa ajili ya wote na kila mmoja akapata na kusaza na kikabaki. Haijalishi mtaji ni mdogo kiasi gani akikishika Yesu ipo nguvu za uzalishaji mkubwa ndani yake.
- Yesu hututimizia mahitaji yetu ya kimwili na kiroho kwa kadri tunavyotaka si kwa kadri anavyotaka yeye. Sisi ndio tunaamua kiasi cha chakula tunachojisikia kula, kama tumeshiba au la, kazi yake Yesu ni kutupatia chakula kwa kadri ya uhitaji wetu.
- Neno la Kristo linaweza kuonekana ni mstari mmoja au maandiko machache lakini ndani yake lina nguvu ya kumshibisha kila mmoja anayelisikia kwa hitaji lake. Tunaona mikate 5 na samaki 2 walitosha kwa wanaume 5,000 na vikabaki vikapu 12. Muhubiri isikusumbue kile Mungu alichoweka ndani yako, kazi yako ni kugawa kama wanafunzi wa Yesu, ni kazi ya Yesu kuhakikisha kile kinachogawiwa ni mkate wake na samaki wake alivyovibariki na hakika vitashibisha mkutano wote na kubaki vilivyosazwa.
Haya mambo 4 ni angalau ya yale tunaweza kujifunza kupitia muujiza ule wa mikate 5 na samaki 2. Hivyo ni matarajio ya Mungu tunapotazama muujiza wowote unaofanyika mahali popote ni lazima utoe ujumbe fulani katika maisha yetu ya kiimani.
Ni kazi yetu sisi tunaosikia habari za miujiza mingi na mara kwa mara kupima juu ya miujiza hiyo kama inaimairisha imani zetu kwa Mungu na kuongeza uhusiano wetu na yeye au la. Hatupaswi kukaa katika hali ya kuutukuza muujiza na kuutafuta muujiza ila tunapaswa kumkaribia sana Mungu katika imani na upendo kwake Yeye pekee na si vile vitu alivyotupatia.
Mungu wetu atusaidie katika kutafakari maneno haya na kutusaidia kusikia sauti zinazoambatana na miujiza au ishara ikiwa zinatuelekeza kwake au la na kujifunza kuchukua hatua sahihi ndani ya Kristo.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
Wako katika Bwana Yesu Kristo
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!