
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘wakasema, Je! Huyu sie Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa anasemaje huyu, Nimeshuka kutoka Mbinguni?Yn.6:42
Mambo ya kujifunza
- Tunaona juu ya wayahudi wanaojua historia ya kimwili ya Bwana Yesu kuhusiana na wazazi wake wakishangazwa na maneno yake ya kwamba ametoka mbinguni. Lakini hawa hawakuwa na ufahamu juu ya historia ya Yesu ya kiroho na jinsi alivyochukuliwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
- Bwana Yesu aliwahi kueleza tofauti ya kuzaliwa katika mwili na ile kuzaliwa katika roho. Akisema kilichozaliwa kwa mwili ni mwili na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Wayahudi walimwona Yesu kama mwana wa Yusufu wakati kwa halisi alikuwa mwana wa Mungu. Sisi tunamwonaje Yesu katika maisha yetu ya kila siku?
- Andiko hili linatupa nafasi ya kujitathmini juu ya utambulisho wetu mbele ya watu au jamii kila siku. Je, watu wanakutambua kama nani? Je unatambulika kutokana na asili yako ya kimwili au ya kiroho?
- Haijalishi historia yetu ya kimwili juu ya wazazi waliotuzaa maana hatukuchagua lakini suala la kuzaliwa kiroho ni uamuzi wetu binafsi kila mmoja wetu. Tunaona fundisho hili la kuzaliwa mara ya pili akilizungumza Yesu mwenyewe kwa Nikodemo na kwamba ndio kigezo cha kuingia au kuishi ndani ya mfumo wa ufalme wa Mungu.
- Watu wengine wanapotosha neno hili juu ya kuzaliwa mara ya pili, lakini hii ndio njia pekee aliyoizungumza Bwana Yesu, ni jambo la msingi kwa kila mmoja wetu ili kurudisha uhusiano wake na Mungu hana budi kuzaliwa mara ya pili au kuzaliwa kwa Roho au kuokoka.
- Watu wanasema wewe u mwana wa nani? Je, wewe mwenyewe kwa nafsi yako unasema u mwana wa nani? Je, Mungu mwenyewe anakushuhudia u mwana wa Mungu au la? Bwana Yesu hakushughulika na jinsi wayahudi walivyomtambua bali alijua yeye binafsi ni mwana wa Mungu kweli?
- Ndugu yangu hatukuchagua kuzaliwa na wazazi tulionao sasa katika mwili ila tumepewa nafasi leo ya kuchagua kuzaliwa katika Roho kwa msaada wa Mungu.
UAMUZI WA LEO
Ikiwa ndani yako ungependa kuona ahadi ya Bwana Yesu inatimia ya kuzaliwa mara ya pili na kwamba unaona uhusiano wako kwa sasa na Bwana Yesu si sahihi na unashuhudiwa moyoni ya kuwa endapo leo ni siku yako ya mwisho kuna uwezekano wa hukumu, basi chukua hatua na kubadili mkondo wa historia yako kwa kusali pamoja nami
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!