
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Kwa kuwa mapenzi ya Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho’ Yn.6:40
Mambo ya kujifunza
- Andiko hili tunaona juu ya ahadi ya Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya kila anayemwamini ya kuwa anapata uzima wa milele. Haya ni mapenzi ya Mungu Baba kwa kila mtoto wake ndani ya Kristo.
- Tunaweza kuwa tumesikia watu wakituhubiria na kutuvutia kwao au kwa mambo au miujiza wanayofanya lakini hawatuelekezi kwa Yesu Kristo. Mwamini unapaswa kuwa na uhusiano wako binafsi na Yesu kwani hakuna mwanadamu atakayesimama kati yako na Mungu.
- Tusiyumbishwe na sauti za watu hata katika dini au madhehebu tunayotumia kuabudu kwa kufuata watu bali tumfuate Yesu Kristo pekee.
- Hatari kubwa ya kuwatazama watu ni pale wanapokutana na changamoto za majaribu basi mwamini naye huanguka kwa kuwa aliweka matumaini ya maisha yao kwa mtu ambaye si Kristo.
- Swali muhimu kujiuliza mimi na wewe siku ya leo, Je ninapokutana na changamoto au shida yoyote ninamtazama nani? Ni wapi ninaanza kutafuta msaada? Maandiko yanatueleza amelaaniwa yule amtegemeaye mwanadamu na kumfanya kuwa kinga yake na moyoni amemwacha Bwana.

- Uzima wa milele hatuupati kwa mtu wala hatufufuliwi kwa matakwa ya mtu bali kwa kigezo cha kumtazama Yesu kila siku na kumwamini katika mambo yote.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!