
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Na mapenzi ya aliyenipeleka ni haya, ya kwamba, katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho’ Yn.6:39
Mambo ya kujifunza
- Andiko hili tunaona juu ya ahadi ya Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya kila amwendeaye kwa moyo wa kuamini kwamba ni ufufuo siku ya mwisho. Ni muhimu kufahamu mpango wa Mungu na hatma ya maisha yetu mara baada ya kutoka hapa duniani. Ni mapenzi ya Mungu kuwaokoa wanadamu wote na pia ni kiu ya Mungu kutufikisha mwisho mwema yaani uzima wa milele.
- Kama Mungu ametujalia kwenda kwa Yesu na kumkubali kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, tuwe na uhakika kuwa atatufufua siku ya mwisho endapo tutaendelea kushikamana naye siku zote. Ieleweke kuwa kuokoka ni mwanzo wa safari na si guarantee ya kufika katika maisha ya uzima wa milele. Hatahivyo kuokoka au kuzaliwa mara ya pili ndio fursa ya awali au hatua ya kwanza katika kufikia uzima wa milele. Tunahitaji kushikamana na Bwana Yesu tangu mwanzo hata mwisho.
- Wakati mwengine sisi waamini maisha yetu hujawa na wasiwasi juu ya safari hii hasa tunapojitazama na kujipima kila siku na kuona hatuna tumaini la kuikamilisha safari hii. Tunakutana na majaribu, ushindani na hata dhambi zinazotusumbua sana. Hii hali isitukatishe tamaa bali inatupasa tuendelee kupambana nayo kwani Mungu anakusudia kila mmoja wetu kufikia mwisho mwema.
- Kwa kula chakula cha kiroho kutoka kwa Bwana Yesu ndani yetu tunajenga tumaini na mtazamo wa tarajio la kufikia mwisho mwema. Ndio maana Bwana Yesu alisema ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe na amekusudia kutufufua siku ya mwisho.
- Kuna dhana ya uongo ambayo imejengeka kwa watu ya kuwa kuna watu Mungu amewakusudia kupotea milele yaani kuingia jehanam kwani Mungu anajua mwisho wetu sisi sote. Dhana hii si kweli kwani neno la Mungu linaeleza wazi ya kuwa Mungu amemkusudia kila mmoja wetu kuingia katika uzima wa milele. Moto wa jehanam ni maalum kwa Ibilisi na malaika zake.
- Ipo njia na mpango maalum wa Mungu kwa ajili yako na kwa ajili yangu wa kutufikisha kwa Mungu salama kabisa tukiwa tumetakasika. Tunapaswa kuendelea kumwomba Mungu na kukaa ndani yake kwa chakula cha kiroho kila siku.
- Tangu sasa tunapaswa kuwa na matumaini ya kwamba bila kujali upinzani uliopo, bila kujali udhaifu wetu wa siku kwa siku, bila kujali dhambi inayotusumbua, bado hatutakufua kwenye dhambi bali tutalala katika utakatifu na Yesu Kristo atatufufua tena na kuishi naye milele.
UAMUZI WA LEO
Ikiwa ndani yako ungependa kuona ahadi ya Bwana Yesu inatimia ya kuwa usipotee milele bali upate kufufuliwa siku ya mwisho na kwamba unaona uhusiano wako kwa sasa na Bwana Yesu si sahihi na unashuhudiwa moyoni ya kuwa endapo leo ni siku yako ya mwisho kuna uwezekano wa hukumu, basi chukua hatua na kubadili mkondo wa historia yako kwa kusali pamoja name
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa. Maandiko yanaeleza wazi ya kuwa
‘Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote’ 1.Yn.1:8 – 9
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!