Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili nifanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka’ Yn.6:38
Mambo ya kujifunza
- Andiko hili tunaona dhahiri ya kuwa Bwana Yesu alikuja duniani kutokana na agizo la Baba wa mbinguni na alikuja kutimiza kile alichotumwa na Baba wa mbinguni.
- Wengi tunaifahamu historia ya mwanadamu pale Edeni jinsi wazazi wetu wa kwanza Adam na Hawa walipoasi kwa kufanya kile walichokatazwa na Mungu. Tangu wakati huo Mungu alikuwa anatekeleza hatua mbalimbali za ukombozi wa mwanadamu. Hatua hizi zilikuja kuhitimishwa kwa ujio wa Yesu Kristo katika mwili yaani Mungu mwenyewe.
- Tangu wakati wa Yesu Kristo kufa na kufufuka hakuna wokovu wa mwanadamu yeyote isipokuwa kwa kupitia Yesu Kristo mwenyewe. Maandiko yanaeleza wazi kuwa Mungu ni mmoja na mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu ni mmoja ambaye ni Yesu Kristo.
- Kazi yote hii aliyoifanya Yesu Kristo pale msalabani ilitulenga mimi na wewe ili tuokolewe kutoka katika sheria ya dhambi na mauti na kuingia katika sheria ya Roho wa uzima.
- Neno linasema ya kuwa Yesu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea. Sisi sote tunazaliwa katika hali ya dhambi haijalishi dini zetu au historia ya familia zetu kuhusiana na Mungu bali kila mmoja anahitaji kujenga uhusiano wake binafsi na Mungu.
- Ni lazima ieleweke ya kuwa haitoshi tu kuzaliwa kwenye dini ukafikiri unao uhusiano na Mungu kutokana na kuwa ‘mkristo’. Paulo alizaliwa kwenye dini ya kiyahudi na akawa farisayo kweli kweli katika elimu ya dini lakini alipokutana na Yesu maisha yalibadilika. Nikodemo alikuwa mwalimu wa dini ya kiyahudi lakini Bwana Yesu alimpa shule ya kwamba mtu hawezi kuingia ufalme wa Mungu pasipo kuzaliwa mara ya pili.
- Lazima ufahamu ya kuwa dini yoyote ile ni juhudi za mwanadamu kumtafuta Mungu lakini WOKOVU ni mpango wa Mungu kumtafuta mwanadamu. Chagua kukaa ndani ya mpango wa Mungu uwe salama.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!