
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe’ Yn.6:37
Mambo ya kujifunza
- Sisi sote tunapelekwa kwa Bwana Yesu kwa mapenzi ya Mungu pekee na wala si kwa nguvu zetu au kutaka kwetu wenyewe. Wengine tumezaliwa na kukuta wazazi wetu katika imani ya kikristo. Tunaweza kufikiri kwa utashi wetu au urithi wa imani ya wazazi wetu tunaamini katika Kristo. Hii si kweli tunajaliwa kumjua Yesu kwa neema yake Mungu wetu.
- Mtu unaweza kuzaliwa na wazazi ambao wameshika imani ya Kristo lakini wewe binafsi usiwe na mahusiano na Yesu Kristo. Jambo hili pia Bwana Yesu aliliona kwa kijana tajiri aliyeshika amri tangu utotoni, lakini alipoambiwa kuuza mali na kumfuata Yesu alihuzunika moyoni.
- Mtu unaweza kuudhuria ubatizo, kipaimara, na ibada zote lakini bado ndani yako usiwe umejenga mahusiano binafsi na Mungu. Lazima tufahamu si kuzaliwa kwetu kwa mwili, au nafasi tulizonazo kwenye Kanisa au jamii bali neema ya Mungu anayotujalia kutukutanisha na Mwanawe wa pekee Yesu Kristo ndio inatupa kujenga uhusiano na Mungu siku kwa siku.
- Bwana Yesu ameahidi ya kuwa kila amwendeaye hatomtupa nje kamwe. Inawezekana katika maisha yetu na kuenenda na Bwana tumekosea, tumeanguka kwa dhambi Fulani, kiasi ya kuwa hata wenyewe tunashindwa kujisamehe, Bwana Yesu anasema kila ajaye kwangu sitamtupa kamwe.
- Tukiamini neno hili tusogee kwenye kiti chake cha rehema ili tupate neema wakati huu kuhuisha roho na nafsi zetu.
- Tusikubali kukaa nje ya Bwana Yesu hata dakika moja zaidi ni hatari sana kwetu. Shetani asituhukumu kwamba hakuna msamaha kwetu, twende kwake kwa njia ya toba atatukubali.
Yesu awakubali
Wakosa, wahalifu,
Waambieni wa mbali,
Habari ya wokovu
Tangazeni kwa bidii,
Akubali wakosa,
Liwe neno dhahiri,
Akubali wakosa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!