Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini’ Yn.6:36
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu anasisitiza katika andiko hili kwa wayahudi na waamini wote pia kumtazama vile anavyojifunua kwao ili wapate kile kinachoambatana na ufunuo huo. Tunaona kupitia ishara ya mikate na samaki, Bwana Yesu alitaka wajue kuwa yeye ndiye chakula cha uzima wa roho na nafsi zao.
- Ni Yesu pekee ndiye anayeweza kutosheleza mahitaji ya utu wa mwanadamu yaani mwili, nafsi na roho zetu. Ishara ya kuwalisha mkate na samaki ilipasa kuwaelekeza wamwone kama chakula cha uzima.
- Sisi tumeona ishara mbalimbali katika maisha yetu hasa kwa habari ya jinsi Mungu anavyotupatia riziki zetu. Tunaweza kufikiri kuwa ni kazi pekee ya mikono yetu ndio tunaishi, si kweli ni Mungu pekee ndiye anayetujalia.
- Fikiri tu kuwa sasa dunia ina watu takribani 7.7 Bilion na wote hawa wanakula chakula chao. Wengine hawana fedha, hali za hewa mbaya au kuna vita n.k lakini wanapata riziki za miili yao. Kama si uweza wa Mungu kutulisha sote ni nini?
- Yesu alituambia tufikiri juu ya ndege au wanyama wote pia hawapandi, hawavuni lakini Baba huwapa chakula cha kila siku. Hii tafsiri itusaidie kujua si kwa juhudi zetu ndio tunakula bali Mungu ametuwekea mazingira ya kupata chakula.
- Tumemwona Yesu kila siku katika riziki anazotupatia kwa ajili ya miili yetu, tumemwona akishibisha ndege, wanyama, samaki na kila kiumbe kila siku, kwa nini hatumwamini kwa ajili ya kutulisha roho na nafsi zetu?
- Kila ulapo chakula cha mwili kuanzia leo kitazame kama ishara ya Yesu kukupa chakula cha uzima, tusiishie tu kutafuta na kulisha miili yetu bali tumtafute Bwana Yesu kwa imani juu ya kutulisha roho na nafsi zetu kila siku.

- Bwana tusaidie kuamini kile ulichotufunulia juu juu yako kuwa wewe Yesu ni chakula cha uzima.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!