
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hatoona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe’ Yn.6:35
Mambo ya kujifunza
- Ni suala moja la kumtambua Yesu kama chakula cha uzima na ni suala lingine kumkubali na kumwendea ili ukipate chakula hicho.
- Bwana Yesu anasema yeye ajaye kwangu hataona njaa kamwe. Je, maisha yetu ya kiroho yanashibishwa siku kwa siku? Je ni wapi unapata chakula cha kiroho kila siku? Ni kwa Yesu au kwa dini fulani, au dhehebu au mtumishi fulani?
- Kuna hali imeingia katika kanisa ambayo inaleta utengano mkubwa sana, waamini wamekuwa wakijitambulisha au kujitofautisha na wengine kutokana na dhehebu, au mahali wanaposali au kwa jina la mtumishi anayewahudumia. Hii si sahihi hata kidogo kwani kama Bwana ni mmoja na Roho ni mmoja haiwezekani tukatofautiana katika chakula tunachokula.
- Paulo alionya tabia hii ya watu kujitambulisha kupitia watumishi kwamba mimi ni wa Paulo au Apolo. Hawa ni watumishi tu lakini sio chanzo cha chakula chetu. Ukiona huna utulivu na mahali unapopokea chakula unatangatanga ujue shida sio eneo bali mtazamo wako juu ya yule anayehusika kufikisha chakula kwako kwamba imani yako umeiweka kwake badala kwa Yesu Kristo na ndio maana hawezi kukushibisha wala kukata kiu yako.
- Hata mtu ukizunguka makanisa yote hakuna mahali au mtumishi anayeweza kukushibisha chakula cha uzima isipokuwa Yesu peke yake. Bwana Yesu alituonya hali hii akituambia ‘watawaambia njoo ufalme wa Mungu uko huku, msihangaike kwa sababu ufalme upo ndani yenu’
- Miito imekuwa mingi sana nyakati hizi na watu wanapenda sana miujiza, si kila wito ni wa kweli au ni wa uongo, unayo kazi ya kupima kabla ya kuamua kwenda. Muhimu sana kumuuliza Mungu aliye ndani yako juu ya aina ya chakula na mahali unapopaswa kukipokea kila siku.
- Ni muhimu kufahamu si kila mtumishi wa Mungu ni kwa ajili yako hivyo hata kama huelewi anachofundisha basi si kwa ajili yako, wapo wengine anatumika kwa ajili yao, wewe muulize Mungu juu ya mahali chakula cha kiroho kwa ajili yako unapopaswa kukipokea kila siku asubuhi.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Amina,ubarikiwe sana mtumishi kwa ujumbe mzuri
Karibu sana brother tuzidi kuombeana ili tuendelee na kazi hii bila kuchoka.