
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji. Ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hatoona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe’ Yn.6:35
Mambo ya kujifunza
- Hatimaye katika maneno haya tunaona Bwana Yesu akijitambulisha kwa Wayahudi kuwa Yeye ndiye Chakula cha uzima. Hili ni jambo jipya kwao kwa sababu hawakuwahi kusikia wala hawakutegemea kusikia. Mstahii huu hasa ndio kiini cha mazungumzo yote ya Yohana sura ya 6.
- Muda wote wa mazungumzo walifikiri kipo aina ya chakula kama kile walichokula baba zao jangwani, lakini mwisho chakula hicho ni Yesu mwenyewe. Ujumbe huu pia ni kwa ajili yetu jinsi ya kumtazama Yesu katika sura na nafasi nyingine anayojifunua kama chakula cha uzima.
- Watu wengi tunamfahamu Yesu kama mwokozi wetu, Bwana wetu au mponyaji wetu, lakini si wengi wanaifahamu sura hii ya Yesu kama chakula cha uzima. Yaani tukimjua Yesu kama chakula cha uzima na kuhakikisha tunakula kila siku chakula chake tunao uzima wetu wa sasa na hata baada ya maisha haya.
- Ili kuona matokeo yoyote ya mambo ya kiroho suala la imani ni jambo la msingi sana. Kama hatuna tafsiri ya kwamba Yesu ni chakula cha uzima hatuwezi kupokea faida zinazotokana na Yesu kama chakula.
- Tunapokea wokovu kwa kuamini juu ya kazi ya Yesu pale msalabani na msamaha wa dhambi tuliopata, lakini kuhusu mfumo wa maisha ya uzima ndani ya Yesu tunapaswa kuupokea kwa kuhakikisha tunaishi kwa chakula cha kiroho ambacho ni neno la Yesu kila siku.
- Watu wengi pamoja na kuokoka kwa muda mrefu hawaoni maendeleo au kukua kiroho, sababu mojawapo kubwa ni kutokuwa na mfumo mzuri wa kupokea chakula cha kiroho kila siku.
- Ukitaka kuona hatua zaidi katika maisha yako ya kiroho na kujenga uhusiano mzuri na Mungu kila siku, basi unapaswa ndani yako kubadili mtazamo na kuanza kutafuta kwanza chakula cha kiroho kitokacho kwa Yesu Kristo ambaye amejitambulisha kwetu kama chakula cha uzima.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Je, una shida ya kusamehe au kushindwa kuomba msamaha?
Basi kama una changamoto ya suala zima la msamaha jiunge na mtandao wetu kwa kujisajili kisha tutakutumia zawadi ya BURE kabisa ya kitabu cha
‘Kwa nini Unalazimika kusamehe?

Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!