Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tulijifunza juu ya Msingi wa Chakula cha Kiroho na kuona juu ya uhitaji wa kila sehemu ya mwanadamu yaani roho, nafsi na mwili.
Leo tunakwenda kujifunza juu ya ‘Nafasi ya muujiza/ishara katika maisha ya kiimani. Karibu sana tuendelee kujifunza.
Nafasi ya Muujiza/Ishara katika maisha ya Kiimani
‘Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula mikate mkashiba’ Yn.6:26
Ufafanuzi
Habari hii ni matokeo ya kile kilichotokea, baada ya Yesu kufanya muujiza wa kulisha watu wapatao 5,000 ambao walikuwa wamemfuata kusikiliza maneno yake kwa kupitia vipande 5 vya mkate na samaki 2. Ndipo makutano hao wakawa wanaendelea kumtafuta Yesu kila alipokuwa anaenda. Soma zaidi (Yn.6:1-25)
Muujiza wa kuwalisha makutano wapatao wanaume 5,000 kupitia mikate 5 na samaki 2, ulikuwa ni ishara ambayo walipaswa kuiona, kuisikia na kuilewa ujumbe uliokuwa unatolewa, lakini hawakuelewa, wao badala ya kujifunza kutoka kwa ishara wakataka waishi ndani ya ishara wakati wote.
Ndio maana tunaona maneno ya Bwana Yesu akiwaambia sababu ambayo wanamtafutia si kwa ajili ya kile walichojifunza ndani ya ishara au muujiza wa kulishwa mkate na samaki bali ni kwa sababu ya kula mkate na kushiba.
Leo, tunataka kuona kwa nini Bwana Yesu alizungumza sentensi hii na inaashiria nini katika maisha yetu hivi sasa.

Ni nini maana ya muujiza?
Muujiza ni tendo/vitendo vinavyofanyika nje ya utaratibu wa kawaida wa kibinadamu katika kufanikisha jambo kwa kusudi fulani. Mfano wa miujiza, kuponya pasipo dawa, kufufua wafu, kulisha mikate, n.k
Katika mfumo wa maisha ya kawaida ya mwanadamu kila jambo lina utaratibu wake wa kulitekeleza. Tunatarajia ili mtu ale chakula ni lazima chakula kilimwe shambani, kitengenezwe kwa maana ya kupikwa kisha kuliwa. Ila chakula kikitokea pasipo kufuata utaratibu huu tunaona ni muujiza. Pia katika utaratibu wa kawaida mtu akiumwa tunatarajia aende hospitali na kupata matibabu kisha kupona lakini mtu akipokea uponyaji pasipo kufuata utaratibu wa kawaida tunaona ni muujiza. Ipo mifano mingi ndani ya neno la Mungu ikionesha juu ya utendaji wa Mungu kupitia muujiza au ishara.
Kusudi la miujiza/ishara
Kusudi la muujiza siku zote ni kutoa ishara au ujumbe ambao unakupa maelekezo juu ya jambo fulani.
Watu wengi wanafurahia muujiza katika maisha yao na wanatamani kila siku maisha yao yawe ndani ya miujiza. Lakini kimaandiko muujiza ni wa sababu maalum na kwa ajili ya kutoa ujumbe kwa aliyetendewa muujiza au walioshuhudia muujiza juu ya habari za Mungu aliyetenda muujiza. Hivyo muujiza si mwisho wa safari bali ni maelekezo juu ya safari na njia unayopasa kuiendea.
Muujiza wowote ambao unaona Yesu amefanya au anafanya hata sasa ni ishara. Maana yake unapaswa kupata ujumbe na maelekezo ndani ya muujiza ule. Watu wengi wanafuata muujiza na wanataka waishi ndani ya muujiza pekee pasipo kuangalia ule muujiza unatoa ishara gani katika maisha yao ya kiroho.
Aina za miujiza
Si kweli kwamba jambo lolote la muujiza yaani kitu kilichofanywa nje ya utaratibu au mfumo wa maisha ya wanadamu kinafanywa na Mungu peke yake. Maandiko yamejaa mifano mingi ya matendo au mambo yaliyofanywa nje ya utaratibu kwa nguvu za shetani. Hivyo ipo miujiza inayofanyika kwa maelekezo na nguvu za Mungu na ipo miujiza inayofanyika kwa maelekezo na nguvu za shetani.
Tuangalie mfano wa miujiza iliyofanywa na watumishi wa Mungu na ile iliyofanywa kwa nguvu za giza
‘BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikilize; kama BWANA alivyonena’ Kut.7:8-13
Habari hii inaonesha dhahiri kile ambacho kilitokea wakati Musa na Haruni walipoenda kutaka ruhusa kwa Farao juu ya kuwaachia wana wa Israel kutoka Misri. Tunashuhudia aina za miujiza iliyofanyika kwa maelekezo ya Mungu na ile iliyofanywa na waganga na wachawi kwa nguvu za giza. Hii inatupa picha sisi wanadamu wa kizazi cha leo kuwa makini sana na miujiza kwani si miujiza yote inatoka kwa Mungu bila kujali imefanyika wapi. Soma habari yote Kutoka.7 – 12 juu ya miujiza iliyofanyika hata Farao kuruhusu wana wa Israel kutoka Misri.
Ninachotaka tutafakari siku ya leo, kama wewe au mimi tungeingia ikulu ya Farao na kukuta nyoka waliotengenezwa kimiujiza yule wa Haruni na wale wa waganga na wachawi, je tungeweza kujua ni nyoka yupi ni ishara iliyotoka kwa Mungu? Jibu ni hapana kwani wote ni nyoka.
Hii ina maana ipo miujiza mingi ambayo watu wanaipokea au wanafikiri inatoka kwa Mungu ila kihalisia ni ishara zilizofanyika kwa nguvu za giza.
Kumekuwa na hali ya watu kupenda muujiza pasipo kumtaka Mungu mtenda miujiza, na miujiza mingi imepoteza watu wengi kwani hata shetani anayo miujiza mingi na anajifananisha na Mungu kwa miujiza yake. Kama vile Musa alifanya miujiza mbele ya Farao na waganga wa Farao walifanya kwa namna hiyo hiyo.
Hivyo usitishike au kushawishiwa na matendo ya miujiza inayofanywa na watu bila kujali vyeo vyao au majina wanayojiita au kuitwa na watu, muhimu cha kufahamu ishara hizo zinakupeleka wapi katika maisha yako ya kiimani.
Maswali ya msingi ya kujiuliza juu ya miujiza au ishara
Ni muhimu sana kwetu waamini kila wakati na kabla hatujachukua hatua juu ya ishara au miujiza tujiulize maswali haya
- Je, muujiza huu au ishara hii ina maana gani au inanielekeza juu ya nini katika maisha yangu?
- Je, muujiza huu au ishara hii inanielekeza kumtukuza Mungu au mwanadamu?
- Je, muujiza huu au ishara hii inaweka vipi uhusiano wangu na Mungu?
- Je, muujiza huu au ishara hii inanishawishi kuitazama yenyewe au kumtazama mtu aliyetumika kufanya muujiza au kumtazama Yesu Kristo?
Haya ni maswali ya msingi sana kuyatafakari kabla hujashawishiwa na ishara yoyote ile bila kujali imetokana na nguvu za Mungu au za shetani. Usikubali kuaminishwa kwa kila ishara hata kama inaonekana imetoka katika madhabahu unayofikiri ni ya Mungu. Ni muhimu sana kulinda moyo wako na imani yako kwani tumesikia madhila mengi kwa watu wengi waliofuata ishara na miujiza wakaharibu imani zao, ndoa zao, familia zao, kazi zao, uchumi wao na maisha yao.
Tunashuhudia kila leo namna mbalimbali za ishara zinazotolewa katika madhabahu duniani kote zikijinasibu kuwa zinatokana na nguvu za Mungu kitu ambacho si cha kweli.
Ni lazima kufahamu juu ya kanuni ya uumbaji ambayo Mungu aliiweka tangu asili ya kwamba mwanadamu ataishi kwa neno lake na si kwa muujiza au ishara. Siku zote ishara au muujiza huja kwa kusudi maalum na huleta taarifa maalum kwa kipindi husika.
Mungu wetu atusaidie katika kutafakari maneno haya na kutusaidia kusikia sauti zinazoambatana na miujiza au ishara ikiwa zinatuelekeza kwake au la na kujifunza kuchukua hatua sahihi ndani ya Kristo.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
Wako katika Bwana Yesu Kristo
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!