
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Makala iliyopita tuliangalia juu ya kuwekaimani kwa Mungu si kwa mwanadamu. Leo tunaangalia kuhusu Chakula cha Kweli.Karibu sana.
‘Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni’ Yn.6:32
Mambo ya kujifunza
- Safari ya wana wa Israel kutoka Misri kwenda Kanaani ni mfano wa safari ya Kanisa lililokombolewa katika Agano Jipya. Tunaweza kujifunza mengi sana kupitia safari hii ya wana wa Israel.
- Kama walivyokuwa wana wa Israel walivyopita vipindi mbalimbali yaani kutoka utumwani kwenda Jangwani na kisha Kanaani, hali kadhalika Kanisa nalo linapita vipindi hivyo vya kutoka utumwani hali ya utumwa wa dhambi, kupita jangwani hapa ni kipindi cha mpito kukua kiroho na hatimaye kuingia au kuziishi baraka za ufalme wa Mungu kama Kanaani.
- Tunajifunza ya kuwa maisha ya Jangwani wana wa Israel waliishi kwa kula MANA katika kipindi cha miaka 40. Mana hii ilitoka mbinguni kila siku ambapo walipaswa kuokota asubuhi. Kadhalika na sisi katika safari yetu ya kumjua Mungu tunahitaji chakula cha kweli au MANA kutoka kwa Bwana Yesu kila siku.
- Kama vile Mungu alivyohakikisha ya kuwa mana ipo kila siku bila kujali hali ya uasi au kiroho ya wana wa Israel vivyo hivyo anatuhakikishia KILA SIKU uwepo wa chakula cha kiroho kwa ajili yako na yangu kutoka kwa Bwana Yesu. Ndio maana andiko linasema ‘…bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni’ neno anawapa ni mwendelezo au kitendo kinachoendelea kila siku.
- Wakristo wanapaswa kuwa waangalifu hasa katika nyakati hizi, kutokana na uwepo wa manabii wa uongo ambao hawatoi chakula cha kweli bali wanatafuta maslahi yao, hivyo kuwafanya watoto wa Mungu kudumaa kiroho na kukaa muda mrefu Jangwani.
- Ukitaka kupima endapo neno unalosikia kama ni chakula cha kiroho au la angalia endapo uhusiano wako na Yesu unaimarika kila siku au unadhoofika. Ikiwa chakula unachopata ni cha kiroho kweli hicho kitakujengea hamu ya kufanya mapenzi ya Mungu na kumtumikia kila siku. Ikiwa neno unalosikia bila kujali ni muhubiri gani au ana sifa gani lakini halikusaidii kuimarisha uhusiano wako na Mungu bali maneno yanayokusukuma kupata vitu au mahitaji tu ya hapa duniani basi kuna changamoto katika ulaji wako.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!