
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Makala iliyopita tuliangalia juu ya uweza wa Mungu kutulisha siku zote. Leo tunaangalia juu ya kuweka imani kwa Mungu si kwa mwanadamu. Karibu sana.
‘Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni’ Yn.6:32
Maneno haya yalisemwa na Bwana Yesu akiwajibu makutano juu ya kauli yao kuhusiana na wazazi wao kula mana kule jangwani kwa mkono wa Musa. Ndipo anawaeleza juu ya kusudi la Mungu kutumia kivuli kile cha agano la kale kwa kuwapa chakula cha kweli kitokacho kwa Bwana Yesu mwenyewe.
Mambo ya kujifunza
- Wana wa Israel waliweka imani kwa Musa kwamba kupitia yeye walipata chakula. Mtazamo wao ni kuwa Musa aliwawezesha kupata chakula kutoka kwa Mungu. Bwana Yesu anarekebisha mtazamo huu kwa kuwaeleza juu ya chakula hicho kuwa ni Yeye aliyeshuka kutoka mbinguni.
- Ni muhimu sana kwetu sisi kujifunza katika neno hili ambalo Bwana Yesu anawaambia hawa makutano ya kwamba si Musa aliyewapa chakula cha mbinguni bali Baba anawapa chakula cha kweli. Watu wengi tunawatazama watumishi Fulani na kuwaona wao pekee ndio wana hati miliki ya imani zetu hii si kweli. Mungu anataka tuondoe mitazamo yetu kwa binadamu hata kama anawatumia kutufikishia ujumbe wake au mahitaji yetu bado anabaki kuwa Mungu.
- Mungu aliweza kutumia kunguru kumlisha Nabii wake mkata wakati wa njaa. Hivyo suala la Mungu kumtumia mtu kukufikishia ujumbe hakubadilishi wala hakupandishi hadhi ya mtu yule kiasi kwamba ukaacha kumsikiliza Mungu.
- Kamwe hatupaswi kutarajia kupata chakula cha kiroho kutoka kwa mwanadamu bali macho yetu yanapaswa kumtazama Yesu aliye chakula cha kweli kishukacho kila siku kama mana kwa ajili ya kuupa ulimwengu uzima.
- Lazima tukumbuke hata Musa aliishi kwa mana ile ile waliyokula wana wa Israel, hakuwa na chakula cha tofauti ni sawa na wengine. Hii itupe picha ya kuwa hata watumishi wanaobeba ujumbe kwa ajili yetu bado nao wanategemea chakula hicho hicho ambacho na sisi tunapatiwa.
- Tafadhali usiweke imani kwa mtu anayetumika kukugawia chakula cha kiroho bali weka imani kwa Mungu anayetupa chakula cha kiroho kupitia watumishi mbalimbali, hii itakusaidia kumwombea mtumishi huyu na itakusaidia na wewe kiasi kwamba hata mtumishi atakapokumbana na changamoto za kiroho na kuteleza au kuanguka imani yako itabaki kuwa imara katika Yesu siku zote.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!