
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Makala iliyopita tunazungumzia uhusiano wa imani na ishara. Leo tunaangalia juu ya uweza wa Mungu kutulisha siku zote. Karibu sana.
‘Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale’ Yn.6:31
Maneno haya yalisemwa na makutano wakitaka kujihakikishia juu ya uwezo wa Bwana Yesu kuwalisha chakula kama Musa alivywalisha baba zao jangwani. Kupitia andiko hili tunajifunza juu ya uwezo wa Mungu kutulisha siku zote.
Mambo ya kujifunza
- Safari ya wana wa Israel ilichukua jumla ya miaka 40 jangwani, hawakulima wala kuzalisha chakula au kufanya biashara lakini Mungu aliwalisha kila siku pasipo kukosa. Tunaona jinsi Mungu akimpa maelekezo Musa juu ya chakula ambacho kitashuka kutoka mbinguni kila siku asubuhi yaani ‘MANA’ ambayo walipaswa kuikota nje kwenye umande.
- Chakula hiki ambacho walikula kwa miaka 40 ndicho kilitunza uhai wao na kuwaokoa na mauti kwa kipindi chote pamoja na malalamiko yao.
- Kupitia mfano huu wa Musa na wana wa Israel jangwani kwa miaka 40 tunajifunza kuwa Mungu ana uwezo mkubwa sana wa kuhakikisha kila mmoja wetu anapata mahitaji yake ambayo si tu ya kimwili bali hata ya kiroho.
- Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuacha kutaabika kwani Mungu anayathamini sana maisha yao, kama ndege wa angani hawapandi wala kuvuna lakini Mungu huwalisha, je si zaidi wao? Hii haimaanishi watu wasifanye kazi ila watu waweke kwanza mtazamo wao na mfumo wa maisha yao katika kutafuta kusudi la Mungu kwanza kabla ya mambo yote.
- Kama Mungu alifanya hivi kwa taifa moja katika kipindi cha miaka 40, kwa nini tunashindwa kumwamini pale tunapopungukiwa na riziki au hitaji fulani kwa muda mchache?
- Tuwe na uhakika na Mungu wetu ambaye ametupatia Bwana Yesu kutupatia riziki zetu za kila siku iwe kwa miili yetu au roho na nafsi zetu maana atafanya bila kujali idadi yetu sisi wote hapa duniani, Mungu ana chakula kwa ajili ya kila mmoja wetu.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!