Day.13. Spiritual Food: Imani kwa Yesu na utendaji wa kazi za Mungu

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Makala iliyopita hii tulijiuliza ‘Unatenda kazi gani ya Mungu?. Leo hii tunazungumzia uhusiano wa imani kwa Yesu na utendaji wa kazi za Mungu. Karibu sana.
‘Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndio kazi ya Mungu, mwaminini yeye aliyetumwa na yeye’ Yn.6:29
Maneno haya aliyasema Bwana Yesu ajibu swali la makutano ambalo waliuliza juu ya utendaji wa kazi za Mungu.
Mambo ya kujifunza
- Tunaona Bwana Yesu akitoa jibu na kuleta tafsiri ya kufanya kazi za Mungu ni kumwamini yeye aliyetumwa na Mungu. Swali muhimu la kujiuliza sisi, je, tunamwamini Bwana Yesu? Kama jibu ni NDIO, je tunaziona kazi za Mungu ndani ya maisha yetu ya kila siku? Je, watu wakitutazama wanaona Mungu akitutumia kama alivyokuwa akimtumia Bwana Yesu?
- Kila mmoja anafahamu juu ya majibu yake mwenyewe kuhusiana na imani zetu kwa Yesu na endapo tunaziona kazi za Mungu akigusa maisha ya watu wengine kupitia sisi au la.
- Kama hatuoni sisi wenyewe kazi za Mungu ndani yetu, je, tunamwamini Bwana Yesu ipasavyo? Ni imani ipi hiyo ambayo Bwana Yesu alisema tumwamini yeye aliyetumwa na yeye? Ni imani ya namna gani ambayo Bwana Yesu anaisema inayotuwezesha kufanya kazi za Mungu?
- Maandiko yanaeleza kwa maneno yake Bwana Yesu kwamba yeye amwaminiye (Bwana Yesu) kazi zile alizozifanya huyo anayemwamini atazifanya pia tena kubwa kuliko hizo. Kama hatuzioni kazi za Mungu ndani ya maisha yetu na kugusa maisha ya watu wengine ni dhahiri imani yetu kwa Bwana Yesu ina upungufu au haijakaa sawa sawa.
- Ni lazima tutofautishe imani ya kumwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu na ile imani ya kutenda kazi pamoja naye. Hizi ni imani tofauti. Watu wengi katika uhusiano wao na Mungu huishia kuokolewa tu hawatafuti zaidi ya hapo, husubiri kifo au unyakuo kwenda Mbinguni. Je, tunamfuata Yesu kwa ajili ya kujihakikishia tiketi ya uzima wa milele kwa sababu tunaogopa Jehanamu? Kama imani yetu imeishia hapa bado tuna changamoto maani inawezekana kabisa baada ya kufika mbinguni na kuwa na uhakika ya kwamba hakuna kwenda jehanamu tunaweza kuachana na Bwana Yesu.
- Imani ya Bwana Yesu kama Mwokozi au Mponyaji haitoshi kutenda kazi pamoja naye, ni muhimu kuendelea kujifunza zaidi na kupata chakula sahihi cha kiroho ili kuingia ngazi nyingine ya kuzitenda kazi za Mungu katika maisha yetu.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!