
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Makala iliyopita tulijiuliza swali la ‘Nani anakupa chakula cha kiroho? . leo hii tunauliza ‘Unatenda kazi gani ya Mungu? Karibu sana.
‘Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yn.6:28
Maneno haya yalisemwa na makutano waliomfuata Yesu wakitaka chakula na alipokuwa akiwaeleza juu ya chakula cha utu wa ndani ndipo wakauliza swali hili.
Mambo ya kujifunza
- Katika makala zilizotangulia tumejifunza juu ya kusudi la chakula katika maisha ya mtu ni kumpa UZIMA na kumsaidia KUTENDA KAZI. Hii ni kweli kwa aina zote za chakula iwe cha mwili au cha utu wa ndani yaani neno la Mungu. Kama mtu hapati chakula anakufa kimwili maana yake uhai wake unaondoka, kadhalika hukiwa hupati chakula cha utu wa ndani unakufa kiroho.
- Upungufu wa chakula cha kimwili huleta udhaifu katika kazi kwa sababu mwili hukosa nguvu vivyo hivyo upungufu au ukosefu wa chakula cha kiroho unaleta udhaifu wa kiroho katika maisha ya mtu kwa kushindwa kutimiza kazi za Mungu.
- Swali muhimu kwako na kwangu, je tunafanya kazi gani za kiroho? Ni kwa namna gani tunamtumikia Mungu? Au tunatumika katika eneo gani linalohusiana na ufalme wa Mungu?
- Kila mtu anaweza kuwa na shughuli yake au kazi yake inayomuingizia kipato na kumjalia kuendesha maisha ya kila siku. Unaweza kujitete ya kwamba natoa sadaka mbalimbali kanisani au kwa watu. Hiyo haitoshi kila mmoja anafanya, je una kitu maalum kwako unachokijua ambacho Mungu amekuelekeza wewe binafsi kukifanya kwa ajili ya kanisa lake?
- Kama hatuna uhakika juu ya ‘kazi za Mungu’ kwa ajili yetu binafsi, ni ushahidi ya kuwa kuna shida katika aina ya chakula tunachokula cha kiroho. Kwa sababu kazi mojawapo ya chakula ni kutuwezesha kufanya kazi za Mungu. Kama hatufanyi inawezekana hatupati chakula kabisa au hatupati chakula sahihi.
- Ieleweke ya kuwa si wote ni wahubiri, au waalimu, au wachungaji au wainjilisti au manabii bali huduma hizi zimewekwa katika kanisa ili kuwajenga watakatifu waweze kutenda na KUTIMIZA HUDUMA ZAO.
- Ipo kazi maalum kwa ajili yako na kwa ajili yangu ambayo unawajibika kuijua na kuifanya kabla ya kuondoka hapa duniani. Suala la kusikiliza kila neno, mafundisho, mahubiri na kila unabii unaoletwa mjini bila kufanya KAZI uliyotumwa au niliyotumwa ni upotevu wa MUDA na RASILIMALI.

- Weka mkazo na msisitizo wa kutafuta chakula kwa ajili yako na kitakachoamsha kiu na njaa ya kutenda ‘KAZI YA MUNGU’ ndani yako.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!