Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Hivyo tutakuwa na mfululizo wa masomo mbalimbali ndani ya Uliza Neno yenye kutuelimisha katika maarifa na hekima ya Kimungu kila siku na kutupatia Chakula cha Kiroho.
Leo tunakwenda kujifunza juu ya msingi wa Chakula cha Kiroho au ‘Spiritual Food’ kwa namna ambavyo Mungu ametutengenezea ili kupata mahitaji yetu ya kiroho kila siku kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Msingi wa Chakula cha Kiroho
‘Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya’ 1.Theth.5:23-24
Maandiko tuluyonukuu ni maneno ya Mtume Paulo akiwaandikia Wathethalonike juu ya nafasi ya Mungu katika kuwakamilisha kwa utakatifu wote. Hatahivyo katika maandiko haya kile ambacho ningependa kushirikiana na wewe siku ya leo ni ufahamu juu ya namna mtu alivyoumbwa au sehemu kuu 3 zinazomfanya mwanadamu.
Maandiko yanaeleza wazi kupitia mistari hii ya kwamba mwanadamu ni zao la sehemu kuu tatu yaani ni roho, nafsi na mwili. Hali kadhalika kila kiungo kinanchomfanya mwanadamu yaani roho, nafsi na mwili vina kazi zake au majukumu yake na namna bora ya kufanya kazi ni kuhakikisha kila kimoja kinapatiwa mahitaji yake.
Wengi wetu tunafahamu sana juu ya mahitaji ya mwili. Kila siku tunaamka asubuhi na kuhangaika kwa lengo la kupata mkate wa siku kwa ajili ya miili yetu. Hatahivyo hatujaweka umakini mkubwa juu ya roho na nafsi zetu zinapataje mahitaji yake ya kila siku.
Ni kazi ya mafundisho haya kuhakikisha pia tunatoa kipaombele kikubwa juu ya roho na nafsi zetu kwa kuhakikisha zinapata mahitaji yake na kurutubishwa siku kwa siku kwa msaada wa Mungu.
Tunaona msisitizo wa Bwana Yesu mwenyewe juu ya kushibisha chakula sahihi utu wetu wa ndani yaani roho na nafsi zetu pale alipokuwa akimjibu Shetani juu ya jaribu la kubadili jiwe kuwa mkate.
‘Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ Mt.4:3 – 4
Hapa tunaona wazi jinsi Shetani alivyojaribu kumtazamisha Bwana Yesu juu ya mahitaji ya kimwili maana alikuwa katika kufunga kwa siku 40 ndipo akaona njaa na mjaribu akamletea jaribu la mkate. Tunaona majibu ya Bwana Yesu akisema juu ya kipaombele chake au kinachopaswa kuwa kwa kila mwanadamu, ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Hii haimaanishi ya kuwa Mungu hataki tule chakula cha kimwili bali anaonesha ni nini kipaombele cha kwanza cha mwanadamu katika ulaji wake. Kwamba inampasa mtu kutafuta au kuweka kipaombele cha kwanza katika kupata chakula cha kiroho kinachohuisha roho na nafsi kwanza kabla ya mwili.

Kila sehemu ya mwanadamu yaani roho, nafsi na mwili zina mahitaji yake ili kuziwezesha kufanya kazi vizuri. Roho ina uhitaji wake, nafsi pia ina uhitaji wake na hali kadhalika mwili nao. Ni muhimu sana kwetu kufahamu na kuweka kipaombele katika kutimiza mahitaji ya utu wetu wa ndani kwanza kwani huo unadumu pamoja nasi mpaka milele tofauti na utu wetu wa nje yaani mwili ni wa kitambo kidogo tu.
Tunaona tena kwa Mtume Paulo akieleza na kuweka msisitizo katika kuhakikisha tunaweka juhudi sana katika utu wetu wa ndani kupitia maandiko haya;-
‘Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku’ 2.Kor.4:16
Paulo anatueleza wazi juu ya bidii tunayopaswa kuiweka katika kuhakikisha utu wetu wa ndani unahuishwa na kujengwa kwa neno la Mungu kila siku. Pia anasisitiza juu ya hali ya utu wetu wa nje yaani miili yetu. Kwa kadri siku zinavyokwenda ndivyo miili yetu inachakaa. Ni dhahiri ya kuwa kila siku tunapoamka tunaikaribia siku yetu ya kifo kuliko jana. Mimi na wewe tu mashahidi juu ya watu wengi ambao tulikuwa nao miaka ya nyuma lakini sasa hatupo nao kwa sababu ya kifo. Miili yao tumeilaza kaburini lakini roho na nafsi zao zinaishi. Je, hatupaswi kujifunza namna bora zaidi ya kuweka nguvu katika utu wetu wa ndani unaoishi milele kuliko utu wa nje ambao ni wa kitambo kidogo?
Mungu wetu atusaidie katika kutafakari maneno haya ya kutuwekea msingi ndani yetu siku ya leo hasa katika kutafuta na kuweka kipaombele katika hitaji la chakula cha kiroho kwa ajili ya roho, nafsi na miili yetu sawa na neno la Mungu.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
Wako katika Bwana Yesu Kristo
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!