
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya changamoto ya Nadharia katika mfumo wa elimu. Leo tunaangalia changamoto Ushindani usio na tija. Karibu sana.
Tunaendelea kuzichambua changamoto ambazo zipo ndani ya mfumo wa elimu na jinsi zinavyoweza kuathiri wanafunzi ambao tunatarajia kuwa wazalishaji katika taifa lolote ili kujiletea maendeleo.
3. Changamoto ya Ushindani usio na tija
Mfumo rasmi wa elimu umejengwa katika hali ya ushindani baina ya wanafunzi binafsi na hata ushindani huo umeenea kwa waalimu na mashule. Nadhani wewe na mimi tunafahamu juu ya matokeo tunayopokea kuhusiana na kiwango cha ufaulu darasani. Kila mwaka tunapokea matokeo na kuelezwa waliofanya vizuri darasa la 7 au kidato cha 4 au kidato cha 6. Tunaambiwa kuhusi ‘Tanzania 1’ na ‘Top 10 students’.
Jambo hili limekuwa likiamsha hisia sana hasa kwa wanafunzi, wazazi na waalimu na shule zao kwa ujumla. Kila mmoja anataka awe wa kwanza au miongoni mwa waliofaulu vizuri sana darasani au shule yake iongoze kiwilaya au mkoa au kitaifa.
Lakini tujiulize maswali ya msingi yafuatayo
- Je, ni kusudi la elimu kuonesha ni nani bora na nani si bora kupitia mitihani?
- Je, wale waliofaulu sana ndio wenye akili sana kuliko wale ambao hawajafaulu sana?
- Je, wako wapi basi wale waliofanya vizuri sana katika kila ngazi yaani darasa la 7, kidato cha 4 na kidato cha 6 katika utatuzi wa changamoto za kijamii?
Maswali haya ninajiuliza si kwa sababu ya kutaka kubeza jitihada za wanafunzi au waalimu au wazazi au shule bali tunapaswa kutazama vizuri juu ya ushindani tunaoujenga kwa wanafunzi una tija yoyote katika maisha yao ya baadae au la. Nitoe mfano wangu binafsi ili nieleweke, elimu ya msingi sikuchaguliwa kwenda shule ya serikali kwa maana nyingine rahisi nilifeli, lakini kidato cha nne nilifanya vizuri sana na kwenda katika moja ya shule za vipaji maalum kwa masomo ya kidato cha 5 – 6, kisha nikafanya vizuri kwa kiwango changu kwenda Chuo kikuu.
Je, mlolongo huu unaonesha picha gani? wapo wanafunzi wengi wanaweza kudhaniwa hawana akili lakini wakipewa nafasi wanaweza kufanya maajabu hapo baadae lakini wapo wanaodhaniwa wana uwezo mkubwa lakini mwisho wa siku matokeo yake si mazuri.
Ushindani tunaoujenga kupitia mitihani na nani ni bora au si bora hauna tija kabisa katika mustakabali wa elimu yetu. Haimaanishi wanafunzi wawe wazembe na wasifanye vizuri bali hatupaswi kutukuza ‘Tanzania One au Top 10’ tunapaswa kuwasaidia kujenga uwezo wa kutatua changamoto za kijamii.
Kama una ushahidi tafadhali nisaidie kwa wale waliofanya vizuri sana katika masomo ikiwa shule za msingi au sekondari wapo wapi sasa na wanafanya nini kwa ajili ya jamii? Majibu nadhani tunayo. Kigezo cha kufaulu mtihani wa darasani hakipaswi kuwa kigezo cha kufaulu maisha na kuleta suluhisho. Tunahitaji kuwajengea wanafunzi dhana ya ushindani katika kutatua matatizo ya watu au uzalishaji wa huduma na bidhaa zenye kuinua uchumi wetu.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!