
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya changamoto ya Ubaguzi katika mfumo rasmi wa elimu. Leo tunaangalia changamoto Nadharia katika mfumo wa elimu. Karibu sana.
Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya changamoto ya ubaguzi ambayo kwa sehemu kubwa imeathiri watu wengi kwa kubaguliwa kwa kigezo cha mitihani ya darasani. Tumeona ya kuwa mitihani haiwezi kwa hakika kutofautisha uwezo wa mtu alionao bali imetukosesha watu muhimu sana wa kuleta mchango kwenye maisha yetu.
2. Changamoto ya Nadharia
Mfumo rasmi wa elimu kwa sehemu kubwa umejengwa na maudhui ya kinadharia au dhana mbalimbali kuliko vitendo. Katika ngazi nyingi ndani ya mfumo rasmi wa elimu wanafunzi wanakaa darasani kwa muda mrefu wakipokea mafundisho kwa njia ya kusikiliza au kusoma vitabu. Tangu ngazi ya shule za msingi mpaka vyuo vikuu zaidi ya 90% ya maudhui au mada zinazowasilishwa kwa wanafunzi zimewekwa katika mfumo wa masomo yanayotolewa kinadharia.
Kitu pekee tunachoona cha vitendo katika mfumo huu wa elimu ni wanafunzi kufanyishwa mazoezi ya kile walichojifunza kupitia mitihani ya kuandika. Mfumo huu unashindwa kuunganisha suala la kujifunza na kutenda kile ambacho tumejifunza. Ndio maana wanafunzi wengi katika mfumo huu rasmi wa elimu hutumia muda mwingi sana kukariri kile walichojifunza na kisha hukitoa kama kilivyo katika mitihani au mazoezi ya mara kwa mara.
Mfumo huu haujaweka namna ya mtu kutumia maarifa au taarifa anazopokea darasani kwa lengo la kutatua changamoto zinazomzunguka au zinazoikabili jamii yake. Wengi tuliopitia mfumo huu tunafahamu kwa hakika si mambo mengi sana tuliyojifunza yanatumika katika maisha yetu ya kila siku. Hii ni kwa sababu tulipokea maarifa au taarifa hizo kwa nadharia na si kwa matendo.
Ni kwa sehemu ndogo sana ya mitaala ya elimu yetu inatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kupitia vitendo hasa pale mtaala unapohitaji wanafunzi husika kwenda katika maeneo ya mafunzo kwa vitendo ‘field attachment’ ambayo mara nyingi haizidi kipindi cha muhula mmoja katika muda wote wa masomo ya mwanafunzi.
Huu ni upungufu mkubwa na haiwezekani kumwandaa mwanafunzi kwa kutumia nadharia zaidi. Tofauti ya wanafunzi walioandaliwa kinadharia na wale walioandaliwa kwa kutumia vitendo utaiona dhahiri mara baada ya kuhitimu masomo yao. Mfano ni rahisi sana wanafunzi waliopitia katika mfumo wa vyuo vya ufundi kama VETA na vinginevyo kupata ajira au kujiajiri kinyume na wanafunzi waliopitia vyuo vya kawaida kwa kusoma nadharia zaidi.
Hivyo kama taifa na bara zima la Afrika tuna kila sababu ya kuhakikisha sehemu kubwa ya elimu tunayotaka ilite mabadiliko katika vizazi vyetu inapaswa kutolewa kwa vitendo zaidi kuliko nadharia. Dhana au nadharia zinabadilika kila siku kutokana na maendeleo hivyo kujikuta wanafunzi wetu wanajifunza vitu ambavyo vimepitwa na wakati. Mfumo Mbadala wa Elimu ‘Alternative Education System’ ndio suluhisho katika kutoa fursa zaidi kujifunza kwa vitendo.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!