
Utangulizi
Moja ya eneo ambalo linaathiri maisha yetu kwa sehemu kubwa ni aina au mfumo wa elimu ambao tumepitia. Mfumo huo unaweza kuwa rasmi au usio rasmi, kwa vyovyote vile aina ya elimu ina sehemu kubwa sana katika kuamua hatma ya maisha yetu. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya changamoto za mfumo rasmi wa elimu sehemu ya utangulizi. Leo tunaanza kuziangalia changamoto moja baada ya nyingine na jinsi zinavyoathiri uwezo wa wanafunzi kujifunza katika mfumo rasmi wa elimu. Karibu sana.
Changamoto kuu
Kama tulivyoangalia katika makala iliyopita juu ya mfumo huu rasmi wa elimu umekuwepo kwa takribani karne 4 yaani miaka 400 iliyopita na kwamba hakuna mabadiliko makubwa sana katika mfumo huu licha ya karibu maeneo mengi ya kimaisha yamebadilika. Hali hii ya kutobadilika ndio inaleta athari kubwa sana kwa kutokupata watu walio na vigezo au viwango vya kukidhi mahitaji ya karne hii ya 21.
Leo tunaingalia changamoto mojawapo ambayo ni Ubaguzi ndani ya mfumo rasmi wa elimu.
- Ubaguzi ndani ya mfumo wa elimu
Dhana ya ubaguzi ni moja ya dhana zinazopigiwa kelele sana duniani, ya kwamba binadamu wote ni sawa wala hawapaswi kubaguliwa kwa namna yoyote ile. Shirika la Umoja wa Kimataifa (United Nations) kupitia tangazo la Haki za Binadamu la mwaka 1948 ambalo ndani yake limebainisha haki mbalimbali za watu ikiwemo ya kutokubaguliwa. Hali kadhalika katiba na sheria mbalimbali za nchi zinatambua haki hii ya kutokubaguliwa kwa mwanadamu yeyote.
Ni kweli kwamba, nchi nyingi zinajitahidi kutoa elimu bure na kuwahakikishia wananchi fursa ya kusoma kwa ngazi yoyote ile. Hapa kwetu tumeona juu ya elimu bure mpaka kidato cha nne na mikopo ikitolewa kwa wanafunzi mbalimbali kwa ngazi za vyuo.
Hatahivyo, bado kwa sehemu kubwa mfumo wa elimu binafsi una mizizi ya ubaguzi juu ya watu pamoja na kuhakikishiwa kwa tangazo la haki za binadamu, Katiba na sheria mbalimbali.
Kipimo cha mtihani kama kigezo cha ubaguzi
Mifumo wa elimu ina ubaguzi kwa kuwachukua baadhi wanaoonekana wanafaulu mitihani na kuwaacha wale wanaoonekana wanafeli.
Sisi sote kwa njia moja ama nyingine tumepitia katika mfumo huu wa elimu ambao ni rasmi. Kiwango cha elimu tuliyonayo sasa ni matokeo ya mitihani tuliyopitia katika ngazi mbalimbali tangu shule za awali, msingi, sekondani na hata vyuoni.
Mfumo huu umejengwa katika namna ya kubagua wale wanaosemekana kufaulu mtihani unaoletwa na mfumo ndio wanaoweza kuendelea wakati wale wanaosemekana kufeli mtihani hawana nafasi ya kuendelea kujifunza. Huu ndio ubaguzi ambao umewekwa na mfumo wa elimu. Tunaweza tusiuone kwa urahisi kwa sababu ni hali ambayo tumeikuta lakini tunapaswa kujiuliza maswali kadhaa kuhusu kigezo hiki cha ubaguzi
- Je, ni kweli wale wasiofaulu mtihani unaoletwa darasani hawana akili?
- Je, wale wanaosemekana wamefaulu mtihani wana akili kuliko wanaosemekana wamefeli mtihani?
- Je, ukiwatazama wale wanaosemekana wamefaulu na wale wanaosemekana wamefeli katika uhalisima wa maisha baada ya shule kundi lipi wana hatua kubwa za maendeleo?
Nadhani majibu yetu tunayo sisi sote tuliopitia mfumo rasmi wa elimu. Sisi ni mashuhuda ya kuwa hata wale waliosemekana hawakufaulu mitihani tunaona wakifanya vizuri katika maisha yao ya kila siku, huku wale waliokuwa vipanga darasani wakipigwa na maisha. Fuatilia wanaomiliki biashara kubwa si wengi wamefika hata ngazi ya digree moja au kidato cha sita, lakini wanawaajiri wale wenye digree zaidi ya moja.
Fuatilia wagundizi wa teknolojia au mitambo au mashine mbalimbali na kiwango chao cha elimu utaona si suala la kufaulu mitihani bali ni uwezo wa utatuzi wa changamoto zilizopo katika jamii.
Ni wazi kipimo cha mtihani wa darasani si halisi sana katika kuamua ni watu gani wanapaswa kuendelea na elimu na watu gani hawafai katika mfumo wa elimu. Tunapaswa kutafakari sana kama taifa lakini kama Bara la Afrika juu ya mifumo ya elimu. Tusipumbazwe sana na kigezo cha mtihani na kuacha wengine wenye uwezo na vipawa vikubwa wasipate elimu muhimu.
Ni lazima tufahamu ya kuwa kipimo halisi cha maisha hakipo katika mitihani bali maarifa ya utatuzi wa changamoto ndani ya jamii. Hivyo tunapaswa kujenga mfumo ambao utaweza kuwapa haki watu wote bila kujali kigezo cha mitihani ya makaratasi kuamua nani ana akili au nani hana akili.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Je, umeziona changamoto za mfumo wa elimu na ungependa kushiriki pamoja nasi katika kufanya mabadiliko na hujui pa kuanzia?
Basi mwandishi anapenda kukushirikisha maarifa haya kupitia vitabu 2 ambavyo vinapatikana sasa kwa mfumo wa nakala tete ambavyo vimesheheni mafunzo kwa ajili ya kusaidia waalimu, walezi, wazazi, wanafunzi kujenga mfumo mbadala wa elimu. Kila kitabu ni Tsh.5,000/-
vitabu hivi vinapatikana kwenye duka la mtandao Get Value.

Kununua kitabu cha Jinsi ya Kujenga Ubobevu Kitaaluma bonyeza link hii
https://www.getvalue.co/home/product_details/jinsi_ya_kujenga_ubobevu__wa_kitaaluma/?ref=kazi_uliza

Kununua kitabu hiki Maarifa ndani ya Taarifa bonyeza link hii, kisha fuata maelekezo ya kufungua akaunti ya mteja Get Value
https://www.getvalue.co/home/product_details/maarifa_ndani_ya_taarifa/?ref=kazi_uliza
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!