AES.4. Ni nini Kusudi la Elimu? – 2

Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wa isaackzake. Pia nikukaribishe katika ukurasa huu maalum kabisa kwa lengo la kufuatilia mambo mbalimbali tunayotarajia kujifunza kwa lengo la kuboresha maisha yetu. Moja ya eneo ambalo linaathiri maisha yetu kwa sehemu kubwa ni aina au mfumo wa elimu ambao tumepitia. Mfumo huo unaweza kuwa rasmi au usio rasmi, kwa vyovyote vile aina ya elimu ina sehemu kubwa sana katika kuamua hatma ya maisha yetu. Katika makala iliyopita tulianza kujifunza juu ya kusudi la elimu. Leo tunaendelea kujifunza zaidi juu ya ‘Kusudi la Elimu’ Karibu
Kusudi la Elimu
Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya mtazamo wa walio wengi hasa kutokana na nafasi ya mfumo wa elimu tulionao sasa elimu inachukuliwa kama mchakato wa kumwandaa mtu kwa ajili ya ajira. Huu ndio mtazamo tunaoona kwa vijana wengi, wazazi na walezi hasa wanapochagiza watoto au vijana juu ya kusoma na kujifunza kwa lengo la kupata ajira. Ndio maana tunaona vijana wakijiuliza mara baada ya kumaliza masomo ya sekondari wanapojiandaa kuingia vyuoni wanataka kujua wasome nini ambacho kinaweza kuwapatia ajira.
Pia tunaona juu ya msisitizo wa Serikali nyingi za nchi za Kiafrika zinatoa kipaombele kwa baadhi ya masomo kutokana na uchache au uhaba wa wataalam katika maeneo haya. Mfano hapa Tanzania kuna kipaombele kikubwa hasa katika masomo ya Sayansi ya kwamba vijana wanaosomea masomo hayo wanapata uhakika wa ufadhili wa Serikali.
Swali muhimu la kujiuliza, je ni kweli au ni sahihi kusema elimu imekusudiwa kwa ajili ya kumwandaa mtu au mwanafunzi kuajiriwa? Je, kihistoria suala la kuajiriwa ndio kusudi la elimu? Je, wakati mfumo rasmi wa elimu haujaingia katika nchi zetu hatukuwa na aina yoyote ya elimu?
Ndugu msomaji, tukirejea ile tafsiri yetu ya maana ya elimu ni dhahiri utaona ya kuwa elimu haikukusudiwa kwa ajili ya kuandaa watu kiajira ila kuwaandaa watu kwa ajili ya maisha.
Tulisema elimu ‘ni kitendo au mchakato wa kupata jumla ya maarifa, kukua kwa uwezo wa kufikiri au kuamua na kujiandaa binafsi kimaisha’
Kwa maana hii tunaona elimu haihusishi mfumo rasmi wa kuingia madarasani pekee bali jumla ya maarifa anayopata mtu kwa lengo la kumwandaa katika safari maisha.
Ni lazima tufahamu ya kuwa kila mtu anacho kitu ndani yake kwa ajili ya watu wengine, elimu inapaswa kukusaidia kuyajua mazingira uliyopo na namna bora ya kutoa mchango wako kwa jamii. Elimu inapaswa kuwa nyenzo ya kukusaidia wewe binafsi kutatua changamoto za wengine kutokana na kitu pekee ulichonacho.
Tatizo la ukosefu wa ajira katika nchi zinazoendelea ni mojawapo ya matokeo ya aina na mifumo ya elimu zetu. Elimu zetu zinaandaa watu wote wafanane wakati kihalisia wanadamu wako tofauti, hivyo tunajikuta tuna watu wengi wenye aina moja ya maarifa wakati uhitaji wa watu hao ni mdogo au hakuna miundombinu sahihi ya kufanya waweze kutumia maarifa hayo.
Ni lazima kila mwanafunzi au mdau wa elimu afahamu juu ya upekee wa kusudi la elimu kwa mtu mmoja mmoja, ni kwa ajili ya kumsaidia kutoa au kuhudumia kile kitu cha kipekee alichobeba ndani yake kwa ajili ya dunia.
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi za mfumo mbadala wa elimu na kujifunza zaidi.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!