
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wa isaackzake. Pia nikukaribishe katika ukurasa huu maalum kabisa kwa lengo la kufuatilia mambo mbalimbali tunayotarajia kujifunza kwa lengo la kuboresha maisha yetu. Moja ya eneo ambalo linaathiri maisha yetu kwa sehemu kubwa ni aina au mfumo wa elimu ambao tumepitia. Mfumo huo unaweza kuwa rasmi au usio rasmi, kwa vyovyote vile aina ya elimu ina sehemu kubwa sana katika kuamua hatma ya maisha yetu. Katika makala ya utangulizi tumejifunza kuhusu ‘Maana ya Elimu’. Leo tunataka kujifunza zaidi juu ya ‘Kusudi la Elimu’ Karibu
Historia ya Elimu
Elimu ni moja ya dhana kongwe kabisa tangu kuanza maisha ya mwanadamu. Katika vipindi mbalimbali mwanadamu amekuwa na namna za kupata maarifa au taarifa zenye lengo la kuboresha maisha yake toka kizazi hata kizazi. Mabadiliko tunayoona kila siku au tuliyojifunza katika historia ya mwanadamu ni matokeo ya aina za elimu ambazo mwanadamu amezipata na kuzitumia kwa ajili ya kuboresha maisha.
Kusudi la Elimu
Pamoja na kuwa maisha ya mwanadamu yamepitia vipindi tofauti vya mabadiliko, hatahivyo KUSUDI LA ELIMU bado linaendelea kuwepo. Inawezekana mifumo ya utoaji wa elimu imebadilika kwa kiasi kikubwa kwa namna ambayo imeathiri hata mtazamo wa watu juu ya makusudi ya elimu.
Tunaweza kujiuliza swali hili pia kama tulivyouliza katika makala iliyopita, je ni nini makusudi ya elimu? Wengi tumezaliwa na kukuta wazazi wetu au walezi wakatuandikisha shule na tukasoma kwa bidii mpaka hatua tulizofikia. Pia na sisi tumepata watoto tunalipa gharama kubwa kuwapeleka shuleni kwa lengo la kupata elimu. Je tunafahamu makusudi hasa ya elimu? Je, tunawaeleza nini watoto wetu wanaoamka kila siku asubuhi kwenda shule kwa nini wanapaswa kufanya hivyo?
Haya ni maswali mazito sana na hatupaswi kujibu kwa mazoea, ni lazima kutafuta kwa kina kiini hasa cha elimu kwa mwanadamu.
Mtazamo wetu wa makusudi ya elimu unaweza ukawa umeathiriwa hasa na aina ya mfumo wa kisasa wa utoaji wa elimu yaani mfumo rasmi wa watu kujifunza kupitia madarasa na mitaala iliyoandaliwa. Wengi huwa na mtazamo juu ya elimu hii ni kuwezesha kuondoa ujinga na kumsaidia mtu kupata kazi au ajira. Tunaweza kuona juu ya mtazamo huu kwa kuangalia aina ya masomo ambayo tumesoma na kazi tunazofanya au masomo wanayosoma watoto wetu na aina za kazi wanazokusudia kuzifanya. Kwa sehemu kubwa tunahusianisha kiwango cha elimu na kazi tunazofanya. Ili mtu awe daktari ni lazima asome masomo ya utabibu, ili mtu awe mwanasheria ni lazima asome masomo ya kisheria n.k
Hivyo tafsiri yetu juu ya elimu kwa kiasi kikubwa inaathiri juu ya mtazamo wetu kuhusu kusudi/makusudi ya elimu. Tunaitazama elimu katika ufinyu wa tafsiri na kuona ni kitendo kile cha kuingia madarasani na kuhitimu ngazi fulani ya mafunzo.
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi katika kufafanua kusudi hasa la msingi juu ya elimu.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!