
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala zilizopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya upimaji unaokosa uhalisia wa utatuzi wa matatizo ya kijamii. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Upimaji kuwa rahisi katika kufanya udanganyifu. Karibu sana.
Msingi mkubwa wa upimaji unaofanywa katika mifumo rasmi ya elimu ni kupima kumbukumbu za mtahiniwa endapo ameweza kuhifadhi mafundisho au mada mbalimbali alizojifunza katika kipindi fulani. Msisitizo mkubwa wa kijamii ni kuona wanafunzi wanapata alama za juu za ufaulu katika mitihani yao bila kujali maarifa ambayo anapaswa kuwa nayo baada ya mafunzo husika. Yule mwenye kufaulu mitihani huthaminiwa tofauti na yule ambaye hakufanya vizuri.
Hali hii hupelekea kuzaliwa kwa tatizo lingine kubwa kwa wanafunzi na hata wakufunzi kuanza kujihusisha na masuala ya udanganyifu au kutumia mbinu zitakazowezesha wanafunzi kufaulu. Hivi karibuni katika mitihani ya kitaifa ya darasa la Nne tumesikia juu ya waalimu kuwatumia wanafunzi wa darasa la sita kuwafanyia mitihani wale wa darasa la nne. Yote hii ni kutaka kuhakikisha shule husika zinafanya vizuri kwa alama za ufaulu na kuvutia wazazi wengi kupeleka watoto wao.
Halikadhalika tumeshuhudia matukio mengi ya wanafunzi kujikuta wanatoa rushwa ya fedha au hata ngono kwa lengo la kuhakikisha wanapata usaidizi au upendeleo katika kufanikisha ufaulu wao.
Upimaji unaozingatia alama za ufaulu unapelekea ushindani wa shule usio na tija, kwani shule zinaacha majukumu ya msingi ya kuwapa maarifa wanafunzi na kuwakaririsha tu taarifa mbalimbali kwa lengo la ufaulu wa alama za juu. Wanafunzi ambao uwezo wao wa kukariri mambo ni mdogo hukataliwa na mfumo huu.
Upimaji wa wanafunzi au kitaaluma unapaswa ulenge hasa katika maarifa anayopaswa kutoka nayo mwanafunzi katika ngazi husika ili kuweza kuwa chachu ya utatuzi wa changamoto za kijamii.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!