
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala zilizopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya upimaji unaofanyika katika muda mfupi kuliko upimaji unaopaswa kuwa kwa muda mrefu. Leo tunaangalia juu ya upimaji unaokosa uhalisia wa utatuzi wa matatizo ya kijamii. Karibu sana.
Upimaji wa wanafunzi kitaaluma unategemea sana juu ya kile walichojifunza darasani na si zaidi ya hapo. Taaluma zinafundishwa kupitia mitaala maalum ambayo waalimu wanapaswa kuikamilisha na kuwapima wanafunzi husika kama wameshika kile walichofundishwa.
Hatahivyo, changamoto au matatizo yaliyopo kwenye jamii ni tofauti kabisa na kile kilichopo kwenye mitaala. Hali hii inasababisha nakisi baina ya kinachofundishwa vyuoni na hali ya matatizo kwenye jamii.
Mfumo wa kitaaluma unahitaji uandishi wa tafiti ‘research papers’ ambazo huwasilishwa ili kuwa sehemu ya upimaji wa ufaulu katika taaluma fulani. Hatahivyo, tafiti hizi zimekuwa zikibaki kwenye makabati ya maktaba za vyuo vingi kwa kukosa uhalisia wa utatuzi wa matatizo ya kijamii.
Tukijiuliza kila mmoja wetu aliyeandika tafiti kama anaweza au ameweza kuifanyia kazi kwenye jamii yake, ni watu wachache sana ambao tafiti zao zipo katika utatuzi wa moja kwa moja wa masuala ya kijamii. Kama sisi hatujaweza kuzitumia tafiti tulizofanya katika kuleta suluhu ya kijamii kwenye matatizo ambayo tulianisha katika tafiti maana yake mfumo wetu wa elimu una changamoto ambayo ni kubwa sana na itaendelea kutafuna rasilimali watu wengi zaidi kwenye bara letu la Afrika.
Dunia tunayoenda nayo kwa sasa ipo kasi sana kwenye mabadiliko, hivyo inatupasa upimaji wa kitaaluma utusaidie kupata suluhu za matatizo yanayotukabili kwa sasa.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!