
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala zilizopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya changamoto ya ya kipimo cha ujumla zaidi kuliko binafsi. Leo tunaangalia juu ya upimaji unaofanyika katika muda mfupi kuliko upimaji unaopaswa kuwa kwa muda mrefu. Karibu sana.
Mfumo rasmi katika ngazi zote una namna ya kupima wanafunzi ili kuwathibitisha katika ngazi husika. Kipimo hiki ambacho kinaweza kuwa mitihani au mazoezi hufanyika katika vipindi maalum kulingana na ngazi husika ya elimu. Mfano masomo ya kitaaluma ngazi ya cheti hutolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja au masomo ya astashahada hutolewa kwa miaka miwili. Hatahivyo, upimaji wake kuonesha mtu amefuzu katika ngazi husika hufanyika kwa muda mchache sana. Tunafahamu mitihani ya muhula au kumaliza mwaka huwa haizidi wiki mbili, na aina ya upimaji wake upo katika nadharia zaidi kuliko vitendo.
Changamoto hii ya upimaji kutumia muda mchache na hasa ukijikita katika kupima uwezo wa kinadharia, ina athari kubwa sana kwa wanataaluma kwani muda mwingi huangaika au kuutumia katika kuhakikisha wanakariri vile walivyosoma ili waweze kufanikiwa kujibu mitihani husika na si kupata utaalam uliokusudiwa katika taaluma husika.
Nguvu kubwa ya wanafunzi na wakufunzi ni kuona wanafaulu mitihani yao na si kutoka na maarifa ya kitaaluma ambayo yangekuwa na msaada ziadi katika kutatua changamoto za kijamii.
Kama taifa na Bara zima la Afrika tunapaswa kusuka mfumo mpya wa elimu ambao utasaidia shabaha ya upimaji wanataaluma wetu ijengwe katika uwezo wa kuonesha namna ya matumizi bora ya maarifa waliyopokea na si kukariri kwa ajili ya mitihani. Upimaji unapaswa kuwa wa muda mrefu na endelevu. Kipimo sahihi kinapaswa kuwa maarifa yanayoonesha namna bora ya kukabiliana na changamoto za kijamii kutokana na taaluma wanazojifunza. Hii itasaidia sana kupunguza tatizo la ajira ambalo linaendelea kutafuna kundi kubwa la vijana ambao wanajikuta wamefanya vizuri katika vyeti lakini katika utendaji hawana wanachokifahamu kwa uhakika.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!