Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala zilizopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya changamoto ya kipimo cha kuangalia alama za ufaulu badala ya uwezo binafsi wa mwanafunzi. Leo tunaangalia changamoto ya kipimo cha ujumla zaidi kuliko binafsi. Karibu sana.
Mfumo wetu rasmi wa elimu umejengwa katika elimu ya jumla katika ngazi zote. Watu wanajifunza kuanzia ngazi ya awali mpaka chuo kikuu mambo ya ujumla. Japokuwa kila mmoja ana utofauti wake, mfumo haujaandaliwa kuzikubali tofauti hizi bali wale wanaonekana wana utofauti wanaondolewa kwenye mfumo.
Upimaji wetu huangalia dhana mbalimbali za kimaarifa kwa ujumla wake na si kuona nji kwa jinsi gani mtu binafsi anaweza kuzielewa au kuonesha uwezo wake katika maeneo tofauti tofauti.
Mfano mtihani wa darasa la saba au kidato cha 4 au cha 6 hufanyika katika ngazi ya taifa bila kujali mazingira tofauti ya kiuwezo waliyonayo watahiniwa au mazingira ya maeneo ya shule walizosoma. Hali hii husababisha jamii kukosa kuona uwezo binafsi wa kila mmoja wetu kwani mfumo unalazimisha wanafunzi wote wajifunze kwa njia moja na wanatarajiwa wawe na uelewa sawia.
Changamoto kubwa inakuja kujitokeza katika ajira au utendaji kazi, ambapo watu wanashindwa kuonesha ubunifu wao au utofauti wao katika utendaji. Kama tulivyojifunza juu ya historia ya mfumo huu, ililenga kuandaa wafanyakazi wa viwandani ambao majukumu yao ni yale yale ya kujirudia mara kwa mara. Lakini sasa kwa maendeleo ya sayansi nafasi nyingi za viwandani zimechukuliwa na mashine na kuongeza uzalishaji zaidi kwa gharama nafuu kuliko kuwa na watu kama rasilimali ya uzalishaji.
Mahitaji ya sasa ya soko la ajira na utendaji kazi yanataka mtu aliyejengwa katika misingi ya kuonesha utofauti na wengine, ubunifu na vipaji katika kukamilisha majukumu yake wakati mfumo wa elimu unawaandaa wanafunzi katika kufikiri na kuamua kama watu walioandaliwa kwa lengo la kufanya kazi viwandani. Ndio maana vijana wetu wengi bado wanapata shida ya kuajirika kwa sababu ya kuandaliwa kiujumla.
Kwa maendeleo ya sasa ya kisayansi, ilifaa zaidi kuwawezesha wanafunzi kufahamu mambo makubwa matatu ya kielimu yaani kusoma, kuandika na kuhesabu kisha msisitizo ungewekwa katika kutambua uwezo wao binafsi na kuandaa mazingira ya kuendelezwa katika maeneo hayo ili kujifunza kwao kuwe na tija, manufaa na ufanisi zaidi kwa jamii. Kama tunavyofahamu tafsiri sahihi ya elimu ni jumla ya maarifa na uzoefu anaojifunza mtu kwa safari ya maisha yake binafsi. Kama kuna aina ya elimu tunayowapa vijana na haina mahali itakapowapeleka katika maisha yao ni upotevu wa muda na rasilimali fedha kwa sehemu kubwa.
Japokuwa tunaisha katika jamii moja, kila mtu ana safari ya maisha yake tofauti na mwengine. Suala la elimu lisiangalie tu kwa sababu mtu amefikia umri fulani bali linapaswa kwenda mbali zaidi kuchunguza ni nini kilichopo ndani ya vijana wetu ndio tuwaendeleze katika maeneo hayo.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!