
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Katika makala iliyopita tuliangalia changamoto ya kipimo kingine ambacho mfumo rasmi huangalia sana juu ya nadharia badala ya vitendo. Leo tunajifunza juu ya changamoto ya kipimo cha kuangalia alama za ufaulu badala ya uwezo binafsi wa mwanafunzi. Karibu sana.
Mfumo wa elimu rasmi na namna ya upimaji wake umejengwa katika kuangalia au kupima kiwango cha alama za ufaulu katika mitihani. Ili mwanafunzi au mtu afuzu kwenda ngazi nyingine ya kielimu ni lazima alama zake za ufaulu katika masomo ziwe juu zaidi ili kupata nafasi. Tunaliona hili kuanzia ngazi za chini sana mpaka kufikia vyuo vikuu mfumo ni huu huu.
Hali hii imeendelea kuathiri sana viwango vya kupima kwa ufaulu wa alama za mitihani hata kwa watoto ambao wapo katika ngazi za shule za awali. Nyakati hizi tunashuhudia watoto wadogo kabisa wanafanyishwa usaili ili kuangalia kama ‘wanafaa’ au wanaweza kujiunga na baadhi ya shule fulani ambazo zinaonekana zina hadhi katika jamii.
Mfumo huu unawajengea hali fulani wanafunzi kutoka ngazi za chini kwa kuhangaika sana kuhakikisha wanapata alama za juu. Wazazi, waalimu, wanafunzi na walezi wanapambana katika kila ngazi kuhakikisha wastani unafikiwa ili kuvuka hatua nyingine. Kwa hali iliyofikiwa kwa sasa mwanafunzi asipokidhi wastani Fulani wa alama haruhusiwi kwenda ngazi nyingine. Tunaliona hili katika darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne, kidato cha sita, mwaka wa chuo kikuu n.k
Ni muhimu sana kufahamu ya kuwa wanafunzi au kila mtu ana uwezo katika eneo Fulani kuliko eneo lingine, na si kweli ya kuwa wale wanaopata alama kubwa zaidi katika masomo ndio wenye akili kuliko wengine. Tunapaswa kufahamu na kujua au kushajiisha wanafunzi wetu kujenga uwezo katika maeneo yale ambayo wana uwezo nayo na wasionekane ni wajinga au waliofeli katika maeneo yale ambayo hawajafanya vizuri. Hali hii ya kimfumo inawaathiri sana kimaisha na kujiona wasiofaa kabisa wala hawana mchango wowote kwenye jamii.
Hali kadhalika tumekuwa tukishuhudia mapungufu makubwa yaliyopo kwa wale wanaosemekana kufaulu kwa alama za juu. Wao wanajenga mtazamo wa kuonesha wanafahamu kila kitu lakini kwa uhalisia wakiletwe kwenye kazi za vitendo hawana uwezo wa kutosha.
Jambo muhimu la kufahamu wakati tunawandaa wanafunzi katika ngazi zote ni kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kuliko ufaulu wa alama za kukariri nadharia. Soko la ajira linahitaji watendaji wenye weledi katika kazi wanazofanya na si wale wenye alama za ufaulu darasani. Sijawahi kusikia watu katika kazi wajivunia daraja la 1 la ufaulu wao wa kidato cha 4 au 6 au ufaulu wao wa kiwango cha juu katika masomo ya chuo kikuu. Waajiri na wateja wanachotaka ni matokeo mazuri katika kazi zao bila kujali kiwango cha ufaulu wako. Kama tuna ufahamu huo sisi kama Taifa, basi ipo haja ya kufikiria upya namna ya uandaaji wa wanafunzi wetu, wajengewe uwezo zaidi katika maeneo wanayoonekana kuyafanya vizuri na wasihukumiwe kwa kunyimwa fursa ya kuendelea zaidi kimasomo eti kwa kigezo tu cha alama za mitihani.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
KITABU KITABU

Je, wewe ni mwanafunzi au mzazi au mlezi au mwalimu na ungependa kupata maarifa zaidi ya kujenga mfumo mbadala binafsi?
Basi mwandishi anakuletea Kitabu maalum ambacho utajifunza kwa undani juu ya Jinsi ya Kujenga Ubobevu wa Kitaaluma
- Maana ya Elimu
- Maana ya Kipimo cha taaluma
- Namna ya kujifunza kitaaluma
- Jinsi ya kujenga Ubobevu wa Kitaaluma
Kitabu hiki kimeletwa kama njia mojawapo ya kuboresha namna ya kujifunza zaidi katika mifumo rasmi ya elimu na kutatua changamoto kubwa ya ajira.
Kitabu hiki kinapatikana kwa nakala tete kwenye duka la vitabu Get Value kwa gharama ya Tsh.4,000/- kubonyeza link hii
https://www.getvalue.co/home/product_details/jinsi_ya_kujenga_ubobevu__wa_kitaaluma/?ref=kazi_uliza
nakala ngumu inapatikana kwa mwandishi 0713 888 040 kwa gharama ya Tsh.5,000/- tu.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!