
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Katika makala iliyopita tulianza kuziangalia changamoto za mfumo wa elimu katika suala la upimaji ambapo tuliona kipimo kinachotumiwa na mfumo rasmi wa elimu ni kuangalia uwezo wa kumbukumbu badala ya maarifa. Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kipimo kingine ambacho mfumo rasmi huangalia sana juu ya nadharia badala ya vitendo. Karibu sana.
Tunaona juu ya mfumo rasmi wa kupima wanafunzi una changamoto kubwa sana ya kuangalia zaidi nadharia kuliko vitendo. Kwa kuangalia kuanzia elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu sehemu kubwa wanafunzi wanapokea mafunzo kwa nadharia na ndio inaangaliwa zaidi kwenye upimaji wa mitihani na hata mazoezi ya mara kwa mara. Mathalani wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ndio wanajenga taaluma zao hupata si zaidi ya miezi 3 ya kujifunza kwa vitendo katika kipindi cha miaka 3.
Changamoto hii inaathiri sana wanafunzi wengi kwa kukosa nguvu kubwa ya ubunifu ndani ya wanafunzi endapo mazingira ya upimaji wao yangejengwa katika vitendo zaidi. Mathalani endapo upimaji wa utaalam kuwa zaidi ya 70% ungejegwa katika utendaji, ingepelekea mabadiliko makubwa sana ya utendaji wa nadharia nyingi na kuibua ubunifu zaidi kwa wataalam.
Karibu kila fani katika ngazi ya chuo kikuu, wanawajibika kuandika utafiti au ‘research’ lakini kwa hakika ni tafiti nyingi sana zinaishia kwenye maktaba za vyuo kwa muda mrefu na kubaki kuwa rejea tu kwa tafiti nyingine zijazo na si vinginevyo.
Kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia, tunapaswa kufikiria upya namna bora ya kuboresha mfumo wetu wa utoaji wa elimu na kuwekeza zaidi katika kufundisha kwa vitendo au kutoa fursa zaidi ya wanafunzi kufanyia kazi yale wanayojifunza kuliko kusubiri kujibu katika mitihani ya kinadharia. Kipimo sahihi cha ufaulu hakipaswi kuwa katika nadharia bali uwezo unaooneshwa kupitia utendaji bora wa wanafunzi. Hii itasaidia sana wahitimu kujiamini zaidi na hata kupata msukumo wa kuanzisha shughuli zao binafsi pindi suala la ajira katika fani zao linapokuwa changamoto.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!