
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala ziliyopita tuliachambua changamoto mbalimbali za mfumo wa elimu kwa ujumla wake jinsi zinavyoathiri sana wale ambao wanatarajiwa kuwa watendaji katika maeneo mbalimbali. Changamoto ya kimfumo imekuwa ni chanzo kikubwa sana kwa wahitimu wengi kukosa uwezo wa kuajirika au kujiajiri. Leo tunaanza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji. Karibu sana.
Ili mwanafunzi aweze kufuzu kutoka ngazi moja ya elimu kwenda nyingine ni lazima atapimwa uwezo wake wa kielimu. Ndio maana mfumo umeweka katika ngazi ya shule za msingi upimaji darasa la 4 na ule wa darasa la 7. Kadhalika upo upimaji kidato cha 2 na kidato cha 4 kisha kidato cha 6. Baada ya hapo mwanafunzi aliyefanya vizuri anaweza kwenda katika masomo ya juu yaani ngazi za vyuo vikuu au vyuo vya kati kulingana na ufaulu wake.
Wadau wengi wa elimu hasa wazazi wamekuwa na hamasa kubwa sana katika kufuatilia suala zima la ufaulu wa alama za mitihani katika mfumo huu wa elimu bila kuangalia au kuchambua athari hasi au chanya za uwepo wa mfumo huu wa upimaji. Ni ukweli ulio dhahiri ya kuwa namna kiwango cha elimu cha mwanafunzi kinavyopimwa kupitia mitihani ndani ya mfumo huu wa elimu haitoshi kuonesha taswira halisi ya uwezo binafsi wa mwanafunzi husika.
Sisi wenyewe tumeshuhudia baadhi ya watu ambao tulisoma nao na wakafahamika kuwa uwezo wao ni wa chini kielimu yaani hawakupata alama za juu, lakini sasa katika masuala ya kimaisha wapo mbali sana kulinganisha na sisi tuliopata alama za juu.
Hivyobasi, tunayo kila sababu ya kufikiri kwa namna tofauti na kujifunza namna bora zaidi za kuweza kurekebisha mfumo wetu wa jinsi ya kuwapima wanafunzi au kuwajengea uwezo wa ziada ili wafahamu kipimo halisi cha uelewa wao au maarifa wanayojifunza shuleni hakipo katika ufaulu wa mitihani ya darasani au mitihani ya kitaifa pekee bali yapo mambo mengine mengi ambayo yanapaswa kuzingatiwa.
Usiache kufuatilia katika makala zinazofuata ambazo zitachambua kwa undani changamoto kubwa ya mfumo wa elimu tulionao katika upimaji wa wanafunzi.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!