
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya changamoto ya mfumo wa elimu kufananisha watu wote. Leo tunajifunza juu ya changamoto ya mfumo wa elimu kuandaa waajiriwa badala ya watenda kazi. Karibu sana.
Tunaendelea kuzichambua changamoto ambazo zipo ndani ya mfumo wa elimu na jinsi zinavyoweza kuathiri wanafunzi ambao tunatarajia kuwa wazalishaji katika taifa lolote ili kujiletea maendeleo.
- Changamoto ya Mfumo kuandaa waajiriwa badala ya watenda kazi
Tuliona katika mfululizo wa makala zilizotangulia juu ya makusudi ya kuanzishwa mfumo rasmi wa elimu ni kusaidia upatikanaji wa rasilimali watu kwa ajili ya uzalishaji viwandani. Hapo awali elimu ilitolewa kwa kufuata mapokeo ya kifamilia na kijamii pasipo uwepo wa madarasa maalum. Hapa maarifa yalisafirishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kulingana na utendaji.
Lakini ulipokuja mfumo mpya wa elimu takribani karne 4 zilizopita mambo yalibadilika katika jamii. Mfumo wa elimu ukaja kuchukua nafasi ya mifumo ya kijamii ya maarifa. Hapa ndipo changamoto kubwa tunazoshuhudia sasa zilipoanzia. Hapo awali hapakuwa na shida ya ajira lakini sasa tunaona mamilioni ya vijana wapo mtaani pamoja na kusoma hawana kazi.
Huu ndio mfumo wa elimu ulioletwa wakati wa ukoloni ili kumsaidia mkoloni kututawala. Ili mkoloni ajihakikishie rasilimali watu kwa ajili ya malengo yake ilibidi kuleta elimu ili watu wajifunze namna ya kutumika na kupata fedha ili walipe kodi. Hali hii imeendelea kurithiwa na tawala zilizofuata baada ya mkoloni kwa kufuata misingi ile ile ya elimu ya kikoloni.
Mfumo huu kwa sehemu ulifanikiwa hapo mwanzo kwa sababu kama mataifa machanga hatukuwa na wataalam wa kutosha katika sekta mbalimbali. Lakini sasa kila eneo lina wasomi wengi sana kiasi kwamba wapo maelfu wanasoma lakini hawana mahali pa kuitumia elimu yao.
Kusema hivi haimaanishi mfumo huu hauna msaada, bali tunapaswa kuuangalia kwa upya ili uweze kuleta tija na manufaa katika nyakati hizi tulizonazo sasa. Kama Afrika tunahitaji namna mpya ya mfumo wa elimu utakaochagiza watu kufanya kazi wenyewe pasipo kutarajia kuajiriwa bali wazalishe wenyewe na kusaidia kuajiri wale waliokosa fursa hiyo.
Kila mmoja wetu anayo kazi lakini si kila mtu anayo ajira. Ipo tofauti kubwa baina ya kazi na ajira. Unaweza ukakosa kuajiriwa lakini huwezi kukosa kazi kama ukitaka kazi. Tunahitaji mfumo wa elimu utakaosaidia kuzivumbua kazi zilizojificha ndani ya vijana wetu katika Bara la Afrika.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Tatizo kubwa ni kuwa mfumo wa Elimu wa sasa unafundisha ubinafsi na mashindano. Tunahitaji mfumo utakaowezazesha wanafunzi kuvumbua uwezo wao, si wakitaaluma bali kiugunduzi na vipaji vyao.
Ni muhimu kuwa na mfumo utakaofundisha kuhoji, kuchunguza, kutafuta ukweli na jawabu la tatizo. Mfumo wa sasa unatoa majibu tu.
Asante kwa chagizo la mada hii
Siku nzuri na njema ikaambatane nawe
Asante sana Brother Alvin mabadiliko huanza na sisi hasa wazazi kama tutachukua wajibu wa kuwasimamia watoto wetu zaidi ya yale wanayopaswa kutimiza shuleni.Tunao wajibu mkubwa wa kuwachagiza watoto kujifunza zaidi juu ya uwezo ulio ndani yao.