AES.11. Changamoto za Mfumo rasmi wa Elimu – Kufananisha watu wote

Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya changamoto ya Masomo Usiyoyahitaji. Leo tunajifunza juu ya changamoto ya mfumo wa elimu kutaka kufananisha watu wote. Karibu sana.
Tunaendelea kuzichambua changamoto ambazo zipo ndani ya mfumo wa elimu na jinsi zinavyoweza kuathiri wanafunzi ambao tunatarajia kuwa wazalishaji katika taifa lolote ili kujiletea maendeleo.
4. Changamoto ya Mfumo kufananisha watu wote
Kama ulifuatilia makala zilizotangulia tuliangalia mada ya asili ya mfumo wa elimu ambapo tuliona ulianza rasmi wakati wa mapinduzi ya viwanda nchi za Ulaya. Hali hii ya mabadiliko ya viwanda ilisababisha kuanzishwa mfumo wa elimu ambao ungehakikisha uwepo wa rasilimali watu kwa ajili ya viwanda.
Zama zimebadilika sana kutoka mapinduzi ya viwanda ambapo viwanda vimeendelea kiasi cha kubadili mfumo wa uzalishaji na hasa kuzalisha kwa kutumia mashine. Tunaona viwanda vikubwa kama vya magari au treni au ndege vinapunguza idadi ya watendaji katika mchakato wa uzalishaji na kuweka mashine. Hali hii imewaondoa watu wengi kwenye kazi za viwanda. Hatahivyo mfumo wa elimu uliosababishwa na viwanda haujabadilika.
Mfumo wa asili wa elimu kwa ajili ya kazi za viwanda ulihitaji wanafunzi wawe na ufahamu sawa sawa katika kila jambo wanalojifunza ili kila mmoja aweze kutekeleza majukumu ya mwengine pindi hayupo. Hali hii ndio inayoendelea katia mfumo wa elimu mpaka sasa. Wanafunzi wote wanajifunza kila kitu pamoja na tunategemea wafanane katika kufikiri, kusema na kutenda kwao.
Hivi unajua msingi wa wanafunzi kuvaa ‘uniform’ ni matokeo ya mfumo wa kufananisha au kutaka kufananisha wanafunzi wote katika kila kitu?
Kile ambacho tunapaswa kufahamu ni kuwa binadamu tupo tofauti kama vile Mungu alivyotujalia, tunavitu tofauti na kuna mambo hatuwezi kufanana. Kutokana na mafunzo tunayopitia katika mfumo rasmi wa elimu, sehemu kubwa ya vipaji vya watu hupotea na dunia inaingia hasara kubwa kwa kupoteza uwezo wa watu kupitia elimu. Tunadhani elimu rasmi ndio mkombozi wa ujinga lakini kwa sehemu kubwa inawatia ujinga wengine kutoweza kutumia uwezo wao wakionekana ni dhaifu na wao kujiona hivyo kwa sababu ya elimu.
Jambo la hakika na la kimaumbile sisi binadamu hatufanani, tunazo tofauti zetu haipaswi mfumo wa elimu kujengwa kwa kutubagua kwa kigezo cha elimu, kila mmoja wetu anao uwezo wake kwenye eneo ambalo ana vipawa vya asili. Muhimu tu mfumo uwape nafasi kila mmoja wetu atoe mchango wake katika jamii, kwa sababu elimu ni maarifa kwa safari ya mtu binafsi na kila mtu ana njia yake.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!