
Utaangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wa isaackzake. Pia nikukaribishe katika ukurasa huu maalum kabisa kwa lengo la kufuatilia mambo mbalimbali tunayotarajia kujifunza kwa lengo la kuboresha maisha yetu. Moja ya eneo ambalo linaathiri maisha yetu kwa sehemu kubwa ni aina au mfumo wa elimu ambao tumepitia. Mfumo huo unaweza kuwa rasmi au usio rasmi, kwa vyovyote vile aina ya elimu ina sehemu kubwa sana katika kuamua hatma ya maisha yetu. Mtandao huu kwa kuona changamoto zilizopo katika mifumo ya elimu, unakuletea ‘Mfumo Mbadala wa Elimu’ au kwa lugha ya kiingereza unaitwa ‘Alternative Education System’ kwa kifupi AES. Hivyo karibu sana katika kuendelea kujifunza hasa juu ya hitaji na malengo ya mfumo huu mbadala wa elimu.
Hitaji ya Mfumo Mbadala wa Elimu
Kila nchi ina utaratibu wake na namna ya kuelimisha watu wake kwa lengo la watu hao kutumika katika kuijenga nchi katika nyanja mbalimbali. Kadhalika Taifa letu na nchi za Afrika tuna mifumo ya elimu ambayo tumekuwa tukiitumia kwa muda mrefu katika kuelimisha watu wetu. Changamoto kubwa ya mifumo hii ya elimu ni kuwa kwa asili haijatokana na nchi zenyewe bali kwa sehemu ni matokeo ya mifumo iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni. Hali hii inachangia upungufu wa namna ya kushughulikia matatizo ya nchi husika.
Halikadhalika mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo tumeyashuhudia katika kipindi cha miaka 20 tangu kuingia karne ya 21 ni makubwa sana. Mabadiliko haya yameathiri mwenendo wa maisha ya mwanadamu katika kila eneo la maisha iwe kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni na hata kiroho. Dunia imekuwa karibu sana kuliko wakati wowote ule. Matumizi ya mitandao, simu za mkononi, usafiri uliorahisishwa, mashine mbalimbali, kwa sehemu kubwa yameathiri nafasi ya wanadamu katika kuhusika na shughuli za kila siku. Mabadiliko haya pia yameathiri ubora wa elimu inayotolewa katika mfumo rasmi kwa maana yamekuwa ya kasi sana kuliko maandalizi wanayopata wasomi. Hali hii imesababisha kuzalisha wahitimu ambao hawana nafasi katika soko la ajira kwa kutoweza kukidhi mahitaji ya soko ya sasa.
Suluhisho
Katika kila changamoto ni lazima itafutwe suluhu. Kila jamii ina namna yake ya kukabiliana na changamoto mbalimbali. Nchi za Afrika zinao wajibu wa kutafuta suluhu juu ya changamoto zinazoambatana na mabadiliko makubwa ya karne hii ya 21. Tunafahamu juu ya nchi za Asia ambazo katika miaka ya 1960 zilikuwa na uchumi karibu sawa na nchi za Afrika lakini kwa sasa zipo mbali sana katika uchumi. Moja ya mkakati wa nchi hizi ni kutafakari upya juu ya mfumo wa elimu kwa ajili ya watu wao. Tunafahamu kwa sehemu tatizo la msingi la nchi zetu ni athari za mifumo ya elimu ambayo tumeirithi na tunaendelea nayo mpaka sasa.
Ndio maana mtandao huu umeleta kwa sehemu juu ya maarifa yanayopaswa kufundishwa kwa watu wetu kama ‘Mfumo Mbadala wa Elimu’ yaani ‘Alternative Education System’ – AES.
Maono
Kujenga rasilimali watu wenye ubunifu na uwezo wa kubadili Afrika na dunia katika Nyanja zote za maisha yaani kiuchumi, kitamaduni, kisiasa na kiroho
Dhima
Kutumia njia sahihi za kupata maarifa sahihi yenye kukidhi changamoto za karne ya 21
Ni nia ya mtandao huu kuchagiza mabadiliko ya kimtazamo kwa kila mwananchi na Mwafrika juu ya kufanya mabadiliko binafsi ya kifikra ambayo yataathiri familia zetu, jamaa zetu, vijiji vyetu na maeneo mbalimbali.
Ni rai yetu kwamba kila mmoja analo jukumu binafsi la kutafakari matokeo ya mifumo ya elimu tuliyonayo na kuanzisha mabadiliko kwa kadri anavyoona inafaa kwa lengo la kusaidia vizazi vyetu vya sasa na baadae. Tunahitaji watoto wetu watoke mitaani na kuingia katika utendaji wa kazi, tunahitaji wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu wawe na uwezo wa kuanzisha shughuli mbalimbali na kuzisimamia. Tunahitaji uhakika wa juu ya uwekezaji unaofanywa na Serikali, taasisi binafsi na hata wazazi katika elimu uonekane una manufaa kwa vijana wetu. Tunahitaji hata wale ambao hawajapata nafasi ya kupita mfumo rasmi wa elimu wawe na ujasiri wa kutoa mchango wao katika kukuza harakati za maendeleo ya Taifa na Bara la Afrika kwa ujumla.
Nikukaribishe katika ukurasa huu wa Mfumo Mbadala wa Elimu ambapo tutakuwa tunajadiliana changamoto mbalimbali na kushauriana namna ya kuboresha maisha yetu kila siku. Karibu sana kwa maoni, maswali, ushauri, mapendekezo n.k
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!