
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili limewakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima’ Yn.6:61 – 63
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu alijua kuhusiana na kukwazika kwa wanafunzi wake kuhusiana na lile neno alilowaeleza kuhusiana na Yeye kuwa mkate wa uzima na kinywaji cha uzima kwa damu yake. Neno hili hawakulielewa ipasavyo na kuona haiwezekani.
- Ni maeneo mengi sana katika maisha yetu tunasikia neno la Mungu ambalo tunashindwa kuendana nalo au kulielewa na hivyo tunatatizika au kukwazika.
- Yapo maeneo kuhusiana na uzazi, mafanikio,kusudi la maisha yetu, huduma zetu, malezi nk ambayo tunashindwa kujua ni kwa namna gani yanaweza kutimizwa katika maisha yetu na kuwa halisi.
- Bwana Yesu anatupa siri kubwa ya Neno lake ya kuwa ni Roho itiayo uzima. Kama tunasikia na kuamini Neno lake basi ndani yetu tunapata uzima au kile kilichoahidiwa ndani ya Neno kinakuwa halisi katika maisha yetu.
- Watu wengi huangalia hali zao za kimwili au mazingira waliyopo sasa badala ya kuangalia ahadi iliyopo ndani ya Neno la Mungu. Ahadi ya Mungu ni hai na ina nguvu ya kufanyika vile ambavyo Mungu amesema.
- Hali ya kimwili tunayoipitia ikiwa ni ugonjwa, ikiwa ni kupungukiwa, ikiwa ni dhiki au hali yoyote inayotusumbua ni suala la muda mchache tu nayo itapita, ila tunapolikubali Neno la Mungu katika mioyo yetu na kuliamini basi tunapokea uzima ulio ndani yake.
- Inatupasa kubadilisha mtazamo wetu kuhusiana na Neno la Mungu kwa kutokufikiri ni maandiko tu ya kawaida na hadithi za zamani bali Neno la Mungu li hai na lina uwezo ndani yake kuumbika ile ahadi ambayo imewekwa ndani yake na kutupa uzima katika Kristo.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!