
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha huko Kapernaumu’ Yn.6:58 – 59
Mambo ya kujifunza
- Ukiifuatilia habari hii na mafundisho haya tangu mstari wa 22 wa mlango wa 6 wa Kitabu cha Yohana, utaona msisitizo aliokuwa nao Bwana Yesu hasa akieleza hitaji la kiroho alilonalo kila mtu.
- Tumejifunza kwa kuangalia kila mstari na ujumbe uliobebwa katika makala zilizotangulia, msisitizo mkubwa umewekwa katika kula chakula ambacho ni mwili wa Yesu au neno lake na kunywa kinywaji ambacho ni damu ya Yesu ili kuwa na uzima.
- Safari ya wana wa Israel kutoka Misri kwenda Kanaani ilikuwa ya maika 40, tunajifunza changamoto nyingi ambazo walipitia katika safari yao. Kile ambacho Mungu aliwahakikishia kila siku ilikuwa chakula kutoka mbinguni yaani Mana waliyokula kwa miaka 40 pamoja na maji waliyopewa njiani.
- Hatahivyo, pamoja na ishara kubwa walizopatiwa, bado wengi wao waliishia jagwani. Ndio maana Bwana Yesu anasema chakula walichokula hakikuwafaa roho zao kilikuwa cha kimwili na hivyo wakafia jagwani.
- Mungu kwa neema yake wakati akiwachukua kutoka Misri kwenda Kanaani hakuwapa tu chakula cha kimwili yaani mana, kware na maji ya kunywa bali alihakikisha ya kuwa wanapata na chakula cha kiroho yaani neno lake au maagizo yake kupitia mtumishi wake Musa.
- Lakini wana wa Israel hawakujali kukipata chakula cha kiroho yaani neno la Mungu lenye kuwafaa katika maisha yao na changamoto zao, waliasi na kwenda kinyume na neno la uzima hata wakaangamia jagwani.
- Kwa mfano wao na mafundisho ya Bwana Yesu tunaweza kujifunza ya kuwa, suala la safari yetu kumfuata Yesu si tu kutoka Misri au kuokolewa, bali tunahitaji kula chakula cha kiroho kila siku mpaka tuingie Kanaani ile ambayo ametuandalia ndani yake.
- Haitoshi tu kuokolewa, bali tunahitaji kulitii neno lake analotupatia kila siku ili kwamba kwa hilo tuweze kuwa na uzima wake milele katika maisha haya na katika ulimwengu ujao. Unaweza kuwa na Bwana Yesu akakutimizia mahitaji ya kimwili na mwisho wake ukafa kama hujatilia maanani mahitaji ya kiroho ambayo ndiye aliyewekwa na Baba kutupatia kila siku.
- Tusimtake tu Yesu anayejibu mahitaji yetu ya kimwili kama chakula, vinywaji, fedha, nyumba, mashamba, watoto, elimu n.k na tukamkataa Bwana Yesu mwenye mamlaka ya kutupa chakula cha uzima. Vitu hivi vya kimwili ni vya muda tu, lakini chakula cha uzima ambacho ni neno lake na damu yake ni vya milele.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!