
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Uandishi wa makala hii umesukumwa hasa na kisa kilichojitokeza hivi karibuni ambacho kilinisikitisha na hata kunifikirisha kile ambacho kinachoendelea muda huu miongoni mwa vijana wengi wa kiafrika kutokana na msongo wa mawazo ya kukosa ajira. Habari hii niliisikia mnamo 3 Februari 2021 katika channel ya Milllardayo kuhusu kijana wa umri wa miaka 28, Sunday Matara kujinyonga kwa sababu ya kukosa ajira. Kijana huyu alikuwa amehitimisha mafunzo ya miaka 3 ya JKT lakini akapoteza matumaini ya kupata ajira ndipo akachukua maamuzi ya kutoa uhai wake.
Kisa hiki kimenitafakarisha maswali kadhaa ambayo ningependa kukushirikisha
- Je, tunawaambia nini vijana wanaoenda shule au kujifunza?
- Je, ni kweli tumaini la mtu katika kujifunza kote kimaisha ni kupata ajira?
- Je, uhai wa mtu unaweza kufananishwa na ajira kwa thamani yake?
- Je, ni sahihi kwa kila asiye na ajira ana haki ya kuondoa uhai wake?
Tukio hili si moja tu, yamekuwepo mengine mengi ambayo tumeyasikia kuhusiana na vijana kukata tamaa ya kimaisha mara baada ya mafunzo yao kwa kukosa ajira.
Kama jamii tunao wajibu wa kuwafunza vijana wetu na kuwaongoza kimaisha ya kuwa sio jambo la uhakika pale unaposoma ya kuwa utapata ajira unayoitarajia. Ukifuatilia makala ambazo nimekuwa nikiandika ya kuwa kila mmoja wetu anayo KAZI ndani yake lakini si kila mmoja wetu anaweza kupata ajira. Kazi ya kila mtu ipo ila ajira ni chache.
Haitupasi kama taifa kuweka matumaini yetu katika ajira bali tunayo kila sababu ya kuwekeza nguvu zetu na maarifa yetu kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kile ambacho kipo ndani ya uwezo wake yaani kazi yake ili atimaye iweze kumwajiri.
Kijana Sunday Matara ni mfano tu wa aina ya vijana wengi waliokata tamaa kimaisha kutokana na hali ya mfumo wa kiajira. Kila kukicha nafasi za kuajiriwa zinakuwa chache licha ya jitihada nzuri zinazofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi bado uwiano wa ajira zinazotengenezwa kulingana na idadi ya vijana haufanani.
Rai yangu kwa vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla ni kuwa elimu wanayoipata iwe ya mfumo rasmi au usio rasmi ni kwa lengo la kuwasaidia kwenda kule ambapo tayari wamechagua au wana ndoto ya kufika huko.
Lakini pia ni lazima tujue ya kuwa sisi wote hatukuja hapa duniani kwa mapenzi yetu wenyewe ila Muumba ndiye aliyeamua tuzaliwe katika familia tulizopita na kupitia mifumo hii tuliyonayo. Kila mmoja anafikia kipindi cha njia panda kwenye maisha yake kwa sababu ya kutokufikia matarajio yake. Sehemu pekee tunayoweza kurudi na kujitafuta kuhusiana na thamani ya maisha yetu ni kwa Muumba wetu pekee maana ndiye anayejua kile tulichobeba kwa ajili ya watu wengine na kinaweza kuleta manufaa zaidi.
Kwa hakika ajira haiwezi kuwa kipimo cha thamani ya maisha yetu kiasi kwamba tunapoikosa tunaona hatuna sababu ya kuishi. Ni kweli nia ya Sunday kama kijana mwengine yeyote kutaka kuleta thamani kwa familia na jamii yake, lakini kuondoa uhai wake bado familia na jamii haijapata tija kutokana na uamuzi huu mchungu bali umeacha majonzi kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla ambayo iliwekeza katika maisha yake.
Uandishi wa makala hii ni kwa ajili ya kusaidia angalau tangu sasa sisi kama wazazi, walezi na vijana kwa ujumla kuchukua tukio hili kama funzo na kwamba lisijitokeze tena katika familia zetu, jamii yetu na taifa letu kwa ujumla. Tuwatie moyo vijana, tusiwawekee matarajio makubwa sana kiasi kwamba wakashindwa kuhimili misukosuko, lakini zaidi vijana tujue iwe kwa ajira au pasipo ajira bado maisha yetu yana thamani kuu sana mbele za Muumba naye ndiye mwenye haki juu ya uhai wetu kwani hatukujileta hapa duniani na wala si jukumu letu kujitoa uhai hapa duniani, ipo sababu kubwa zaidi ya sisi kuwepo hapa siku ya leo bila kujali changamoto tunazozipitia wakati huu.
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!