Purpose 5. Hatua za kujua kusudi – Tafuta maarifa kuhusu kusudi la maisha

Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi. Katika makala iliyopita tuliangalia kuhusu hatua ya pili ambayo ni kutengeneza kiu au shauku ya kutaka kujua kuhusu kusudi la maisha yako.
Leo hii tunakwenda kuangalia hatua ya tatu ya kujua kusudi la maisha yako. Karibu sana.
Hatua ya 3 –Tafuta maarifa kuhusu kusudi la maisha
Kiu au shauku ya kufahamu kuhusu kusudi la maisha haitoshi peke yake bali unahitaji zaidi maarifa kwa kujifunza kuhusiana na makusudi ya maisha. Ni lazima kuanza kutafuta taarifa sahihi na mahali sahihi zinazoweza kukusaidia kupata mwangaza kuhusiana na maisha yako juu ya kile ambacho Mungu amekusudia wewe ufanye katika maisha haya.
Watu wengi wanapopata watoto na kuanza kuwalea huweka msisitizo sana katika elimu ya darasani au elimu rasmi. Familia na Serikali huingia gharama kubwa sana kuhakikisha ya kuwa kila mmoja anapata elimu bora kwa lengo la kumsaidia kujikimu kimaisha.
Hatahivyo, jamii au familia haziweki msisitizo mkubwa zaidi katika kuwaongoza watoto au vijana katika kufahamu ni nini hasa wamekuja nacho ndani yao kwa ajili ya kutimiza kusudi la maisha yao. Hivyo watu wengi hujikuta wanatumikia makusudi ya Serikali au familia zao kwa sababu ndio maarifa waliyojazwa tangu utoto wao.
Mungu amemwekea kila mmoja wetu nafasi ya kupata maarifa ya kweli kutoka kwake kama tukikubali kujifunza kutoka kwa neno lake. Yapo majibu ya maswali yako binafsi kwenye vitabu vya maandiko matakatifu. Watu hufikiri ya kuwa vitabu hivi havina maana kwa sasa kwani vimeandikwa miaka mingi iliyopita, lakini kwa hakika maandiko haya yana uwezo wa kukufungulia njia ya kufahamu kusudi la maisha yako.
Tuangalie maandiko yafuatayo ambayo yanaweza kukuhekimisha katika kufahamu kusudi la maisha yako;
‘Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.’ Zab.139:16
‘Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo’ Efe.2:10
Mungu aliyetuumba sisi sote anatufahamu tangu mwanzo wetu na hata mwisho wetu. Tunaona katika Zaburi anavyoeleza juu ya kutufahamu kabla hatujaumbwa lakini pia tayari siku zile ambazo zimeamriwa juu yetu kabla hatujaanza kuziishi tayari zilishaandikwa katika vitabu vyake. Pia tunaona ya kuwa kuna aina ya mwenendo au matendo ambayo Mungu alishayatengeneza kabla ya sisi kuwepo ambayo tunapaswa kuenenda nayo. Huu ni ufahamu mkubwa sana ambao tunapaswa kujifunza ya kupata elimu sahihi kutoka kwa Mungu mwenyewe kuhusiana na taarifa sahihi za maisha yetu binafsi. Pata muda weka bidii katika kujifunza kila siku ni makusudi gani ambayo umekuja kuyatimiza katika maisha haya.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!