
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi. Katika makala iliyopita tulianza kuangalia hatua ya kwanza katika safari ya kulifahamu kusudi la maisha yako ambayo inasema ni Kutambua mamlaka iliyo juu.
Leo hii tunakwenda kuangalia hatua ya pili ya kujua kusudi la maisha yako. Karibu sana.
Hatua ya 2 –Tengeneza kiu ndani yako
Baada ya kufahamu juu ya uwepo wa mamlaka ya juu kuhusiana na maisha yako, jambo muhimu kabisa linalofuata ni kutengeneza kiu ndani yako kuhusiana na kutaka kujua kuhusu kusudi la maisha yako.
Kama tunavyofahamu suala la kufahamu kusudi la maisha ya mtu si watu wengi wana ufahamu nalo lakini inawezekana mtu kujua kusudi lako kama utaweka nia thabiti au kiu ndani yako ya kutaka kujua kuhusu kusudi la maisha yako.
Watu wengi wanatoa kipaombele cha maisha yao katika kujifunza juu ya elimu rasmi au kuhusiana na vipawa vyao au masuala ya biashara na uzalishaji mali, lakini si wengi wanaoweka nguvu zao au utashi wao katika kutaka kujua kuhusiana na kusudi la maisha yao binafsi.
Changamoto hii ya watu wengi kutokufahamu habari za makusudi ya maisha yao inaweza kuchangiwa na sababu nyingi ikiwepo suala hili kutokuzungumziwa katika nyumba za ibada. Mara nyingi katika imani tunazojifunza hatupati mafundisho kuhusiana na kusudi la maisha yetu ila tunafundishwa namna ya kujenga uhusiano na Mungu ili tukifa tuweze kufika kwake.
Tuangalie maandiko yafuatayo katika kujenga nia au kiu ndani yetu;
‘Haya kila aonaye kiu njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani. Isa.55:1
‘Nawe utakusudia neno, nalo litadhibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako’ Ayu.22:28
Kwa maandiko haya tunaweza kuona kiu au dhamira au nia ya kutaka kupata kitu ina nguvu sana katika maisha ya mtu na kuweza kuleta matokeo yaliyotarajiwa. Endapo mtu ataweka nia thabit katika kutaka kujua kuhusiana na kusudi la maisha yake basi atalifahamu tu. Ukiweka kusudi ndani ya moyo wako ya kuwa unahitaji kulifahamu kusudi la maisha yako basi kwa hakika utapata kulijua. Hii ni hatua muhimu sana ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuijua na kuifanyia kazi. Weka nia yao au tengeneza kiu katika maisha yako ya kutaka kulifahamu kusudi la maisha yako kutoka kwa Mungu aliyekuumba kwani ndiye pekee mwenye kufahamu juu ya sababu hasa ya wewe kuwa hapa duniani.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!