AES.14. Kipimo cha kumbukumbu badala ya maarifa

Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulianza kuzichambua changamoto za mfumo wa elimu katika upimaji, kwa kuangalia kiujumla mojawapo ya changamoto kubwa ya mfumo huu rasmi ya elimu. Leo tunaanza kuzichambua changamoto zinazoonekana katika mfumo wa upimaji. Karibu sana.
Ipo tofauti kati ya uwezo wa kutunza kumbukumbu na uwezo wa kutoa maarifa yanayotokana na elimu. Mfumo wetu rasmi wa elimu kwa sehemu kubwa umejengwa katika kupima uwezo wa kumbukumbu za wanafunzi na si kiwango cha maarifa waliyopata kutokana na elimu waliyopokea. Wale ambao wana uwezo wa kukumbuka kile wajichosoma basi wana nafasi kubwa zaidi ya kufaulu mitihani yao.
Chukulia mfano mitihani ya elimu ya msingi ya darasa la 7, kwa siku 2 wanafunzi wanafanya mitihani ya kuhitimisha elimu nzima ya miaka 7. Mfumo wa maswali wanayoletewa ni wa kujaza majibu ambayo wanachagua hapo hapo yaani ‘multiple choice’ hali hii hupelekea ufanyaji pia uwe wa kubahatisha. Hali kadhalika hata mifumo ya upimaji ngazi za juu bado kwa sehemu kubwa maswali hayahusishi kuoanisha elimu waliyopokea na changamoto zilizopo ndani ya jamii.
Elimu wanayopata wanafunzi katika ngazi yoyote inapaswa kubadilishwa kuwa maarifa kwa maana mtu aweze kuitumia katika kukabiliana na changamoto za kijamii ambazo zinamzunguka. Mhitimu wa ngazi yoyote iwe elimu ya msingi, sekondari au chuo kama atashindwa kuitafsiri elimu yake katika kutatua changamoto za kijamii bado haijaweza kuzalisha maarifa ya kutosha.
Fuatilia kipindi ambacho wanafunzi wametangaziwa mtihani au zoezi utaona nguvu kubwa wanayotumia kusoma vitabu, notes, vitini n.k hii ina maana wanafahamu ya kuwa upimaji unazingatia zaidi uwezo wao wa kukumbuka walichosoma na si maarifa yatokanayo na walichojifunza. Hii ina athari kubwa sana kwetu kama taifa tunajikuta tuna wahitimu wengi ambao hawana maarifa ya kutusaidia utatuzi wa changamoto zetu.
Kama wewe ni mzazi au mlezi una kijana aliyehitimu shule ya msingi au sekondari au chuo, muulize kama ana uwezo wa kufanyia kazi yeye binafsi kile alichojifunza shuleni au la? Wengi wao watakuambia hakuna ajira au hawana mtaji n.k
Tunapaswa kuanza kufikiria upya namna ya upimaji wa wanafunzi wetu katika ngazi mbalimbali ili tusizalishe watu wenye kukariri taariza za kielimu bali watu wanaotoka na maarifa ambayo watayafanyia kazi baada ya elimu husika.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!