Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Mimi ndimi chakula cha uzima’ Yn.6:48
Mambo ya kujifunza
- Katika andiko hili tunaona kwa mara ya pili Yesu Kristo akijitambulisha kwa wayahudi kuwa wewe ndiye chakula cha uzima. Katika sura hii ya 6 kwa mara ya kwanza katika mstari wa 35. Na sasa anarudia tena neno lilo hilo kuhusiana na yeye kuwa chakula cha uzima.
- Unapoona mtu anarudia mara kwa mara katika mazungumzo jambo lile lile ina maana aidha wanamsikiliza hawajamwelewa kile anachozungumzia au ndani ya kauli ile kuna ujumbe wa ziada wanaopaswa kuuona au kuusikia wasikilizaji wake.
- Kama tulivyojifunza tangu awali katika makala hizi za chakula cha uzima, msisitizo umekuwa katika kumfahamu na kumjua Yesu Kristo kama chakula cha uzima au chakula cha kiroho au chakula cha watu wote kulisha utu wao wa ndani.
- Tunakula kila siku kwa ajili ya miili yetu, tunahangaika kila siku kutafuta chakula na mpaka sasa tuna mazoea baadhi ya vyakula. Kitu kikubwa ambacho kwa bahati mbaya si watu wengi wanafuatilia kile kinachofanyika ndani ya miili yao hasa baada ya kupokea chakula husika. Wengi wanakula ili kuendelea kuishi wasife na njaa lakini si kwa lengo la kuimarisha miili yao na kuleta matokeo mazuri ya matumizi ya nguvu zinazotokana na chakula.
- Msingi wa kula vyakula bila kufuatilia athari chanya au hasi ndani ya miili yetu ndio husababisha maradhi mengi sana kwa sasa katika maisha ya watu wengi. Magonjwa mengi ambayo yamekuwa yakikatisha uhai wa watu ni matokeo ya kula vyakula visivyo na mchango chanya katika miili yao. Tuna magonjwa mengi ambayo yanasababishwa na chakula au tabia za ulaji wetu.
- Ni lazima tufahamu kitu muhimu kinachopaswa kufanywa na chakula ndani ya mwanadamu ni kumwezesha KUISHI na KUFANYA KAZI au kupata NGUVU za kufanya kazi katika majukumu yake. Kama chakula unachokula iwe kimwili au kiroho hakina mchango wa kukusaidia kuongeza siku zako na kukuwezesha kufanya majukumu yako kwa ufanisi basi mwisho wa chakula hicho ni udhaifu na hatimaye mauti.

- Maandiko yanatueleza hapa ya kuwa Yesu Kristo anasema yeye binafsi ni chakula cha uzima. Hii ina maana kama tunahitaji maisha ya kiroho na kama tunataka kuona Mungu akihusika na maisha yetu na majukumu yetu ya kila siku basi tunamuhitaji Yesu kama chakula cha uzima.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!