
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona changamoto ya Kiburi. Leo tunaangalia changamoto ya vipaji vingi.
Sababu 6. Changamoto ya Vipaji vingi
Wapo watu ambao wamejaliwa vipaji zaidi ya kimoja. Mtu anaweza kuwa na vipaji viwili au vitatu mpaka vitano kutokana na mahitaji na makusudi ya maisha yake. Tunawaona watu hawa kila kitu anaweza kufanya. Watu hawa wanaonekana na uwezo mkubwa kwenye jamii na kuwa tegemeo katika maeneo ambayo wana vipaji husika.
Hatahivyo, baadhi yao huishia katika maisha mabaya kwa sababu ya vipawa vyao. Badala ya vipawa vyao kutumika katika kuwasaidia jamii au kunufaika pia wao binafsi, vipawa vyao vinatumika vibaya na kuleta madhara kwa jamii na wao binafsi.
Wapo watu wana uwezo mkubwa wa kufikiri au wa kutengeneza vifaa mbalimbali lakini wanaweza kuutumia ujuzi huo na vipaji hivyo kuleta madhara ya kimaisha na hata ya kiuchumi kwa watu wengine. Wapo wazungumzaji wazuri lakini wanaishia kuwa matapeli, wapo mafundi wazuri lakini wanaishia kutengeneza silaha za kudhuru binadamu wengine. Wapo wataalamu wa mifumo ya kiteknolojia lakini wanaishia kusaidia kuiba fedha na mali za watu wengine.
Hii ni changamoto kubwa sana ambayo kwa sasa dunia inakumbana nayo ya ukosefu wa maadili kwa watu wenye uwezo mkubwa au vipaji vingi. Hali hii pia hupelekea wao kutoishi maisha ya manufaa kwa jamii na wao kwa ujumla kuishia kufungwa au kupoteza uwezo wao katika kunufaisha jamii.
Pia uwepo wa vipaji vingi kwa mtu kama hajajifunza vizuri elimu kuhusu vipaji kunaweza kusababisha ashindwe kuzalisha ndani ya jamii kwa kutokujua ni nini cha kufanya. Mtu mwenye kipaji kimoja ana nafasi kubwa ya kufanya makubwa na kufanikiwa kwa sababu ana eneo moja ambalo atawekeza nguvu zake huko ili kupata matokeo, lakini wale wenye vipawa vingi hawana cha kushika bali wanagusa hapa kidogo na pale kidogo hivyo hawapigi hatua kubwa.
Ni muhimu sana endapo ukajifahamu una kipawa zaidi ya kimoja basi weka utaratibu wa matumizi ya vipawa hivyo na mwombe Mungu akuongoze namna ya kuvitumia ili visilete madhara kwa jamii na kwako pia.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!