
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona changamoto ya Kutonoa kipaji. Leo tunaangalia changamoto ya Kiburi.
Sababu 5. Changamoto ya Kiburi
Kipaji ni kitu kizuri na kipaji kinakupa mtu kukubalika katika maeneo mengi. Mwenye kipaji ni mtu wa thamani katika jamii yake na pia ana wafuasi wengi. Hatahivyo kipaji kinaweza kukuletea changamoto kubwa ya kiburi au majivuno kiasi kwamba sifa ya mtu mwenye kipaji ikaharibika na kupoteza mvuto kabisa kwa watu.
Hili jambo si geni kabisa katika jamii yetu na hata duniani tumeweza kuwashuhudia watu wenye uwezo mkubwa walivyoanza na kufikia kiwango cha juu ya ubora wa vipaji vyao lakini ghafla wakaanguka na kusahaulika katika nyanja za vipaji vyao. Watu hawa wapo katika kila eneo ikiwa ni mpira, masumbwi, riadha, mpira wa kikapu, wanamuziki, waigizaji, waandishi n.k
Mtu anapokuwa na nguvu ndivyo anavyoweza kudhihirisha wajihi wake au ‘character’ yake halisi kuliko alipokuwa hana kitu. Jambo muhimu ambalo watu wanye vipaji na kazi zao zinapata kibali katika jamii wanalopaswa kujifunza ni kuwa wanyenyekevu wakati wote. Kwa kadri kipaji kinavyokupeleka juu machoni mwa watu ndivyo unavyopaswa kuendelea kujishusha ndani ya moyo wako kila siku ili uendelee kukua zaidi.
Sifa ambazo wamekuwa wakipata watu wenye vipaji kutoka kwa mashabiki au watu wa karibu au watu wanaonufaika na vipawa vyao, zimekuwa sumu kubwa sana kwao kiasi cha kubweteka na kuona wamefikia kila wanachotaka na hakuna cha kufanya tena zaidi ya hapo. Wenye vipaji wanajiona ya kuwa hakuna anayeweza kufikia mafanikio walioyonayo hivyo hawana haja ya kuweka kazi zaidi na kuendelea kunoa vipaji vyao. Huu ni mtazamo hasi ambao unawarudisha wengi nyuma na mara wanasahaulika kabisa kwenye jamii. Wengi wanaishia kusema ‘enzi zangu ilikuwa hivi na vile’ hawana tena ushawishi wa watu na kuleta athari chanya katika jamii.
Tumeshuhudia tabia hasi zianaambatana na watu wenye vipawa kama matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, mahusiano yasiyo ya uhakika, ugomvi n.k tabia zote hizi zinatokana na aina ya kiburi inayojengeka kutokana na mafanikio yaliyoletwa na vipaji.
Hivyo katika mambo ambayo yanaweza kukusaidia kutunza kipaji chako katika kipindi unapojifunza zaidi na kukinoa ni lazima kujifunza tabia njema au mipaka utakayojiwekea katika kipaji chako ili hata utakapofanikiwa uwe umejiandaa kitabia na kisaikolojia mafanikio yasikusababishie kiburi na hatimaye kuanguka.
Pamoja na kujenga kipaji chako hakikisha unajenga tabia njema ya kuendana na kipaji chako ili ukitumie kwa muda mrefu zaidi.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!