
Utangulizi
Katika mwendelezo wa makala hizi za Mtazamo wa Kiroho kuhusu Corona Virus (Covid – 19) tunaona juu ya dunia nzima kuingia katika mashaka makubwa kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu. Changamoto kubwa imeendelea kuwa ukosefu wa tiba au chanjo ya kumaliza ugonjwa huu. Kila mmoja yupo katika hatua za kujiadhari kutokana na ugonjwa huu na wito upo duniani kote kutafuta suluhisho. Kila sekta ya kimaisha imeathiriwa kwa sehemu kubwa, hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. Nchini kwetu Tanzania tunaendelea kuchukua taadhari ili kupunguza kasi ya maambukizi. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. Makala ya iliyopita tulianza kuangalia hatua za kushughulikia pigo kwa kuichambua hatua ya 1 inayozungumzia ‘aina na asili ya adhabu’. Katika makala ya leo tunangalia juu ya Hatua ya 2 inayohusu ‘Waathiriwa wa adhabu’. Karibu tujifunze.
Hatua ya 2
Chunguza juu ya nani waathiriwa wa adhabu?
‘BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimepachagua kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa’. 2.Nya.7:12 – 15
Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya kuchunguza aina ya adhabu na asili yake, hatua hii ya 2 inazungumzia juu ya kutambua au kuchunguza ni akina nani waathiriwa wa adhabu husika.
Kwa kutazama jinsi pigo ambalo kwa sasa dunia nzima ipo kwenye maumivu yaani Corona. Ni dhahiri pigo hili limewahusu watu wote, bila kujali dini, madhehebu, kabila, itikadi, jinsia, rangi, umri au hali za kimaisha. Tumesikia athari zake kwa mataifa madogo kwa makubwa, matajiri kwa masikini, kwa walio makanisani na misikitini na hata wapagani.
Ukisoma mazungumzo ya Mfalme Sulemani ya 2. Nya.6 anazungumzia maombi kwa ajili ya taifa la Israel ambalo linatambulishwa kama ‘watu wa Mungu’ na majibu ambayo Mungu anampatia katika 2.Nya.7:13 – 14 anazungumzia endapo atapeleka adhabu kwa ‘watu wake’ ambao ni taifa la Israel.
Kwa muktadha huu wa historia ya ukombozi wa taifa la Israel wakati wa Agano la Kale unafananishwa na Kanisa la Kristo katika Agano Jipya. Tunapojifunza yale Mungu aliyofanya pamoja na wana wa Israel ni kivuli cha mambo halisi ambayo Mungu anatembea na Kanisa lake katika Agano Jipya. Tunaona udhihirisho huo katika maandiko haya;
‘Sasa basi ikiwa mtatii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli’ Kut.19:5 -6
‘Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema’ 2. Pet.2:9 – 10
Maneno haya tuliyonukuu yanadhihirisha juu ya nafasi ya Kanisa katika Agano Jipya kama vile nafasi ya Israel katika Agano la Kale. Ndio maana watu wa Kanisa wana ujasiri wa kunukuu maneno ya 2.Nya.7:13 – 14.
Changamoto kubwa ya Kanisa la sasa
Changamoto kubwa ambayo inalikumba Kanisa la sasa ulimwenguni pote bila kujali mipaka ya mataifa ni hali ya watu wa Kanisa kutamani kufanikiwa na kubarikiwa sana kama lilivyofanikiwa au kubarikiwa taifa la Israel. Sehemu kubwa ya waumini wa kikristo wanapenda kujifananisha kwa masuala ya Baraka na mafanikio kama taifa la Israel. Nyakati hizi tumeona zaidi wakristo kutoka duniani kote wakitembelea taifa la Israel na kujifunza mambo kadhaa ya kuongeza imani zao na uhusiano wao na Mungu wao. Hili ni jambo zuri sana na linapaswa kuendelezwa.
Hatahivyo, linapokuja suala la MABAYA, LAANA au ADHABU hapo wakristo wengi utasikia ya kuwa hizo laana zilimalizika msalabani, au mabaya hayatatupata kama wale wa Agano la Kale kwani sisi ni wa Agano Jipya au hatuwezi patwa na adhabu kama zile za Agano la Kale. Hapa ndipo napata shida na wasiwasi juu ya aina ya imani yetu katika Kanisa.
Kuna kitu kinatafsiriwa vibaya na hakijaeleweka vizuri katika Kanisa yaani NEEMA YA MUNGU ina maana gani na utofauti wake na SHERIA YA MUSA au TORATI. Wakristo wengi wanafikiri kuja kwa Bwana Yesu kuliiondoa TORATI au SHERIA YA MUSA, na kwamba ukiwa na UHUSIANO na Bwana Yesu unaishi ndani ya NEEMA hivyo unaweza kuishi tu kiholela. Huu ni uongo ambao utaweza kupoteza watu wengi tu hapa duniani. Maneno ya Bwana Yesu mwenyewe yanadhihirisha ukweli huu juu ya uwepo wa torati kama alivyosema;
‘Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie’ Mt.5:17 -18
Bwana Yesu aliweka wazi kwa maneno yake mwenyewe juu ya uwepo wa torati na zaidi sana Yeye kuja kuitimiliza na si kuitangua. Ni kwa namna ya kipawa cha Neema ambayo mtu anaipokea na uwepo wa Roho Mtakatifu kumwongoza ili kuitimiza torati.
Kinachosemwa na maandiko ni kuwa kwa kuja kwake Yesu, yale ambayo yalipaswa kutekelezwa kwa sheria ya Mungu ambapo yalishindikana, ndani ya Yesu, waamini wanapewa uwezo mpya wa kushinda na kutimiza sheria ya Mungu kikamilifu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Mtume Paulo anaeleza katika barua kwa Warumi akisema;
‘Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho’ Rum.8:1 – 5
Maandiko haya tunaweza kuona
- Kuna hukumu ya adhabu kwa watu walio nje ya Kristo
- Kuwa ndani ya Kristo Yesu hakumaanishi KUOKOKA bali kuishi kwa kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu
- Sheria inayofundishwa na Roho Mtakatifu ndani ya mtu ndiyo inamuweka mtu huru mbali na sheria ya dhambi na mauti
- Hata kama mtu ‘ameokoka’ lakini anafuata MWILI basi sheria ya dhambi na mauti inafanya kazi ndani yake na kwa mantiki hiyo yu nje ya Kristo
- Mtu ambaye yu nje ya Kristo Yesu kwa sababu ya mwenendo ipo hukumu ya adhabu
Si suala la kuishi KIHOLELA kwa sababu UMEOKOKA. Nieleze wazi ya kuwa KANISA au watu wa Mungu katika Agano Jipya tunaweza KUHUKUMIWA SASA na KUADHIBIWA kwa sababu ya mwenendo wetu.
Ukweli ni lazima usemwe katika Kanisa hata kama unatuhusu sisi binafsi au sisi wote, muhimu sana kwetu ili tupone. Tusipende kusikiliza sana taarifa za kufarijiana ya kuwa hayatatupata mabaya wakati kwa hakika ndani yetu hatufuati utaratibu wa Roho Mtakatifu. Kusema hivi haimaanishi waliopata magonjwa haya ni waovu sana bali itupe sisi ambao bado hatujapata maambukizi ya kuwa si WATAKATIFU sana, tuna kazi ya kufanya toba kwa ajili yetu na wengine pia, maana wakati wa ghadhabu hauangalii mdogo wala mkubwa, tajiri au masikini.
Mimi sijui kuhusu injili ya watu kuishi kiholela imetokea wapi au ya kwamba siku hizi hatuna haja ya kufuata maagizo ya torati? Naomba mtu wa Mungu utafakari maneno haya ya Bwana Yesu kisha uniambie ni kipindi gani kina sheria kali kati ya torati au kipindi hiki cha neema?
‘Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza ndugu yake itampasa jehanam ya moto’ Mt.5:21 – 22
‘Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake’ Mt.5:27 – 28
Ndugu yangu hii ni mistari ipo ndani ya Biblia, swali langu kwako na kwangu mimi mwenyewe wakati Bwana Yesu akichambua torati ya Musa na Neno lake kwa watu wa Agano Jipya, kati ya sheria hizi mbili ipi ni kali? Je, ya agano la Kale ndani ya Torati au sheria za Agano Jipya ndani ya Neema?
Jibu unalo wewe na mimi.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia leo. Tunakushukuru kwa Neno lako la uzima jinsi ambavyo limefunua udhaifu wetu ya kuwa hatuhesabiwi haki kwa sababu tu ya kuokoka bali kuishi katika utaratibu wa Neema yako ndani ya Sheria ya Roho Mtakatifu kila siku. Tunakusihi utujalie moyo wa toba ya kweli tusidhani ya kuwa wasio wakristo ndio waovu kuliko sisi bali sisi tutumike katika kuleta upatanisho wetu binafsi na wewe na kisha tuwe sehemu ya kuwafikia wengine kwa moyo wa toba, katika Jina la Mwana wako Yesu Kristo utusikie na kuturehemu. Amen
# Sauti ya Matumaini # Toba ya Dunia
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!