
Utangulizi
Katika mwendelezo wa makala hizi za Mtazamo wa Kiroho kuhusu Corona Virus (Covid – 19) tunaona juu ya dunia nzima kuingia katika mashaka makubwa kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu. Changamoto kubwa imeendelea kuwa ukosefu wa tiba au chanjo ya kumaliza ugonjwa huu. Kila mmoja yupo katika hatua za kujiadhari kutokana na ugonjwa huu na wito upo duniani kote kutafuta suluhisho. Kila sekta ya kimaisha imeathiriwa kwa sehemu kubwa, hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. Nchini kwetu Tanzania maambukizi yamekuwepo na pia vifo vimetokea. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. Makala ya utangulizi nimeeleza nini hasa kusudi la makala hizi na namna mimi na wewe tunapaswa kuchukua mtazamo gani ili kushiriki kutoa suluhisho. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Mamlaka ya Neno la Mungu. Karibu tujifunze.
Mamlaka ya Neno la Mungu
Waamini katika Yesu Kristo wanapaswa kuifahamu mamlaka kuu katika maisha yao na hatma za maisha yao ipo katika NENO la Mungu. Wakati huu ambapo kila mtu ni mtaalam wa afya, kila mtu ni kiongozi, kila mtu ana weledi katika kila eneo ni lazima Kanisa liweze kujua namna ya kusikia vizuri. Habari hasi zimekuwa nyingi mno, lawama zimekuwepo kila upande, hakuna matumaini tena si kwa walimwengu wala Kanisa la Mungu.
Kwa kiasi kikubwa ulimwengu na hasa Kanisa (waamini katika Yesu Kristo) wameondoa macho yao katika uweza wa NENO la Mungu na kutumaini hekima za kibinadamu au maarifa ya kibinadamu. Kutokana na mafanikio makubwa yanayoshuhudiwa kila kukicha katika sayansi na teknolojia ulimwengu umejitenga kabisa na misingi ya NENO la Mungu na kudhani kila tatizo linaweza kutatuliwa kwa fikra za kibinadamu au uwezo wa kisayansi.
Kwangu mimi kuandika makala hizi ninaweka msimamo wangu juu ya MAMLAKA YA NENO la Mungu ndiyo mamlaka ya mwisho yenye kueleza kila dhana na kila hitaji na kila SULUHISHO analotaka mwanadamu. Mtazamo huu utasaidia sana kutokuyumbishwa na upepo wa kila elimu ambao unapita sasa na kusambaa kila kona. Ieleweke ya kuwa kusema hivi haimaanishi tunapaswa kupuuza miongozo ya kiafya inayotolewa na mamlaka za Serikali, la hasha. Kusema hivi inamaanisha tuko katika mapambano ya kutafuta SULUHU ya shida iliyoingia duniani, pamoja na kuzingatia miongozo ya kiafya tunayopewa na mamlaka husika. Wapo wanayasansi wanafanya majukumu yao duniani kote, tuendelee kuwaombea Mungu awape hekima na maarifa ya kweli katika kutatua shida hii. Lakini pia Kanisa linao wajibu wa kuchukua hatamu za kuongoza ulimwengu kutafuta suluhisho la kiroho kwa janga hili.
Kwa nini Neno la Mungu ndio mamlaka ya juu?
- Neno la Mungu ndilo lililoumba mbingu na nchi na vitu vyote
‘Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri’ Ebr.11:3
- Neno la Mungu ndilo limewekwa kuratibu mifumo ya maisha ya wanadamu na viumbe vyote
‘Hii ndio jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu’ Muh.12:13
- Neno la Mungu ndilo limebeba majibu ya changamoto zozote wanazopitia wanadamu vizazi hata vizazi
‘Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao’ Zab.107:19 – 20
- Neno la Mungu lina uwezo wa kuchunguza jambo lolote na kulidhihirisha asili yake na makusudi yake
‘Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu’ Ebr.4:12 – 13
- Neno la Mungu ndilo silaha iliyopewa Kanisa kushinda changamoto zozote
‘Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo’ 2 Kor.10:3 – 4.
‘Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si ju ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwasababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote kusimama….tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote’ Efe.6:10 – 18
Hizi ndizo kwa uchache sababu 5 kwa nini mimi binafsi naamini katika MAMLAKA YA NENO LA MUNGU juu ya kila kitu kuwa ndiyo mamlaka ya juu zaidi. Zipo sababu nyingi ambazo zimeanishwa katika maandiko ambazo unaweza kuzichunguza wewe binafsi. Sababu hizi na nyingine zitusaidie sisi Kanisa kuweka fikra zetu na mitazamo yetu sawa sawa na kile Mungu anachoeleza KUHUSU MAMBO YOTE ndani ya maandiko. Kwa hakika hata suala hili tunalopitia dunia nzima lina maelezo yake kimaandiko tukilichunguza.
Nakusihi ndugu yangu katika Kristo usiwe msomaji na mtazamaji tu katika hili CHUKUA HATUA madhubuti katika kushiriki kutafuta uso wa Mungu na NENO lake kwa ajili ya kutuvusha kipindi hiki kigumu.
Bwana Yesu aliwahi kusema juu ya watu kupotea kwa kutokuyajua maandiko
‘Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu’ Mt.22:29
Kwa tafsiri ya kiingereza maneno haya yanaweza kusomeka ‘….You are wrong/in error/mistaken/deceived because You don’t know what the Scriptures teach and you don’t know anything about the power of God’
Kwa nini Kanisa tupotee? kwa nini na sisi tunaimba wimbo mmoja na ulimwengu? Wakati Bwana Yesu alitupatia Roho Mtakatifu kwa ajili ya kutuelekeza kwenye kweli yote na kutupasha habari ya mambo yajayo? (Yn.16:12 – 15)
Hivyobasi, katika mfululizo wa makala hizi nitakuwa nikitumia maelezo yanayopatikana katika maandiko matakatifu kuelezea kiini, sababu na asili ya changamoto hii ambayo imeikumba dunia. Mungu aendelee kutubariki na kutuwezesha kwa neema yake.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia. Kwa fikra zetu, maneno yetu na matendo yetu tumekukosea kwa kusikiliza hekima za kibinadamu na kuacha kukutazama wewe na NENO lako. Tumejawa na hofu badala ya tumaini, mashaka badala ya IMANI. Tunakuomba uturehemu na kutusamehe kwa kutokuliangalia NENO lako ambalo ndilo asili yetu na asili ya kila kitu, ndilo lina maelezo yote ya kutuwezesha kuvuka salama katika shida hii. Tujalie kurudi kwako na uweza kwa kuyaelewa maandiko na nguvu zako. Roho Mtakatifu uliyemtuma anifunulie mimi (………………………………………..) kuyafahamu makusudi yako na mapenzi yako na kuweza kuchukua hatua madhubuti kutafuta suluhisho la kweli. Tunakuomba utujalie haya kwa utukufu wa Jina lako na mwana wako Yesu Kristo. Amen
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!